Ili kuwa na maisha bora kabisa unayoweza kuwa nayo, unahitaji vitu hivi viwili muhimu;
Kitu cha kwanza ni kujua maamuzi sahihi na bora kabisa kwako.
Kitu cha pili ni kuwa na ujasiri wa kuyafanya maamuzi hayo licha ya ugumu na changamoto utakazokutana nazo.
Mambo hayo ni rahisi kuyasema, lakini ugumu wake upo kwenye kuyafanyia kazi.
Na wala usianzie mbali, anza na wewe mwenyewe, anzia hapo ulipo sasa.
Kwa sehemu kubwa, maisha unayoishi sasa siyo yale unayoyataka, unajua kabisa kwamba unaweza kuwa na maisha bora zaidi ya uliyonayo sasa na unajua ni hatua zipi unapaswa kuchukua, lakini kutokana na ugumu au changamoto zilizopo mbele yako, unaahirisha maamuzi na hatua hizo.
Yaangalie maisha yako na utajionea mwenyewe maeneo mengi ambayo unajua kabisa ni maamuzi gani unapaswa kuyafanya, lakini mpaka sasa hujayafanya.
Kisha jua ni hofu gani inakuzuia kufanya maamuzi hayo.
Ukishajua hofu hiyo, jenga ujasiri wa kuivuka. Kumbuka mara zote hofu huwa inaondolewa kwa kuchukua hatua na siyo kufikiri au kusubiri.
Hivyo angalia ni hatua zipi unazoweza kuchukua ili zikuondolee hofu ya kufanya maamuzi ili uweze kufanya maamuzi sahihi kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,