“Try to be the master over greed, sloth, lechery, and rage.” – Leo Tolstoy
Tulijifunza ushindi mkubwa na udumuo ni ushindi juu yako mwenyewe.
Je ni vitu gani unavyopaswa kuvishinda kwako ili uwe na maisha bora?
Vipo vingi, lakini muhimu vya kuanzia ni hivi;
Ishinde tamaa na ulafi, hivi vinakuangusha kwa kuhangaika na mambo yasiyo na tija yoyote kwako.
Ushinde uvivu, ndiyo kitu pekee kinachokuzuia usipige hatua, maana unajua unachotaka kufanya, umeshapanga kabisa kufanya, ila wakati wa kufanya unafika, uvivu unakukaribia na unaahirisha kufanya, hapo uvivu unakuwa umeshinda. Usikubali.
Shinda uzinzi, huu unapoteza muda wako, nguvu zako na mwisho wa siku unakuacha na aibu na kujidharau wewe mwenyewe. Tamaa ya mwili inakusukuma kufanya jambo ulilofikiri litakupa raha, lakini baada ya kufanya inapelekea ujidharau. Ushinde uzinzi kwa kishindo kikubwa.
Ishinde hasira, hii ndiyo baba lao, maana hutajua imeingia saa ngapi bali utayaona madhara yake baada ya kuwa imeondoka.
Hasira inakunyemelea, inatawala akili yako, inakusukuma ufanye mambo, halafu mwisho unajiambia kwa nini umefanya.
Ishinde kwa kutoruhusu ikuingia na kama itakushinda kwenye kuingia basi ishinde kwa kutokufanya chochote pale unapokuwa na hasira.
Kwenye kijitabu chako andika leo nakweza kushinda TAMAA, UVIVU, UZINZI na HASIRA kwa kishindo kikubwa.
Sitokubali vitu hivi vinitawale, bali mimi nitavitawala leo na kila siku ya maisha yangu.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania