Umewahi kujiuliza kwa nini baadhi ya mabishano huwa hayana manufaa yeyote kwa anayeshiriki kwenye mabishano hayo?
Chukulia mabishano ya dini, siasa na michezo, maeneo ambayo watu wanakuwa na ubishani kila siku.
Watu wanaweza kubishana sana kuhusu dini (mfano Ukristo na Uislamu), lakini mwisho wa siku hakuna anayebadili dini yake kwa sababu upande wa pili umetoa hoja nzuri.
Kadhalika kwenye siasa (mfano CCM na Chadema) au michezo (mfano Simba na Yanga) watu wanaweza kutumia muda mwingi na nguvu nyingi mno kubishana, lakini mwisho wa siku kila mtu atabaki kwenye upande wake.
Kitu kimoja kinachopaswa kukushangaza ni nini inapelekea hiyo? Kwa nini watu wawe tayari kubishana wakati wanajua mabishano hayo hayawezi kuleta tofauti yoyote kwao na kwa wale wanaobishana nao?
Hapa ndipo tunapopata jawabu kwamba tatizo ni ITIKADI.
Maana ya Itikadi.
Itikadi (Ideology) ni mkusanyiko wa imani unaoshirikiwa na kikundi cha watu fulani.
Maana hiyo ya itikadi inatupa vitu viwili muhimu sana vinavyofanya itikadi iwe changamoto kwa wengi.
Kitu cha kwanza ni imani, kwenye itikadi yoyote ile, huhitaji kuwa na kigezo cha elimu, uelewa, kipaji au hata kufikiri kwa kina. Kitu pekee unachohitaji ni kuamini, na mtu yeyote anaweza kuamini chochote.
Kitu cha pili ni kikundi cha watu, itikadi haijakamilika kama haina kikundi cha watu wanaoishikilia. Na hili ndiyo linafanya itikadi ziwe hatari kwa sababu watu wanaacha kutumia akili zao kufikiri na kufuata kundi linafanya au kusimamia nini.
Kwa nini itikadi ni mbaya?
Kama tayari una itikadi kali, umeshaikataa makala hii tangu mwanzo, ukijiambia kwamba maisha hayawezi kwenda bila itikadi, na huo ndiyo ubaya wa itikadi, unaharibu akili ya yule anayeishikilia.
Ukishakubali itikadi, maana yake umejiambia hutafikiri tena kwenye jambo hilo na hapo unakuwa umeacha kuwa binadamu kamili.
Iko hivi rafiki, kitu pekee kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe wengine ni uwezo wetu wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi kulingana na hali tunayokuwa nayo kwa wakati huo. Lakini unapokuwa na itikadi kali hairuhusu hilo kutokea, hupati nafasi ya kufikiri, wewe unaangalia tu wengine wanafanya nini na kisha kufanya hivyo pia.
Mchwa huwa wana tabia ya kufuata mchwa alie mbele yake, hivyo mchwa akishaona kuna mchwa mwingine mbele yake, hakuna kingine anafanya, bali kumfuata. Hivyo ukitaka kuua mchwa, wafanye watengeneze duara, hapo mchwa hao watazunguka kwenye duara hilo mpaka wafe kwa njaa, kwa sababu kila mmoja anamfuata mwingine, bila ya kujiuliza kufuata huko kunampeleka wapi.
Hivi ndivyo binadamu tunavyojiangamiza pale tunaposhikilia itikadi kali. Kuna jambo ambalo kwa fikra za kawaida kabisa ungeweza kufanya maamuzi sahihi, lakini kwa sababu ya itikadi unalazimika kufanya kisichokuwa sahihi.
Itikadi inaharibu akili yako.
Charlie Munger, bilionea mwekezaji na mmoja wa watu wenye hekima kuwahi kuwepo hapa duniani, anasema itikadi huwa zina tabia ya kukomaa kadiri mtu anavyozitumia.
Kwenye moja ya hotuba zake, Munger ananukuliwa akisema; When you’re young it’s easy to drift into loyalties and when you announce that you’re a loyal member and you start shouting the orthodox ideology out, what you’re doing is pounding it in, pounding it in, and you’re gradually ruining your mind. So you want to be very, very careful of this ideology. It’s a big danger.
Hapa Munger anamaaanisha; unapokuwa kijana, ni rahisi kuangukia kwenye itikadi fulani na pale unapojitangaza kwamba wewe ni mwanachama mwaminifu wa itikadi fulani na kuanza kuhubiri itikadi hiyo, unachofanya ni kuzidi kuingiza itikadi hiyo kwenye akili yako na mwishowe unaharibu akili yako. Unapaswa kuwa makini sana na itikadi, ni hatari kubwa.
Hili liko wazi, kadiri mtu anavyoanza kuhubiri itikadi fulani akiwa kijana, ndivyo anavyozidi kuiharibu akili yake mwenyewe. Anajikuta akifanya mambo siyo kwa sababu ndiyo sahihi kwake kufanya, bali kwa sababu ndicho ambacho anajulikana kufanya.
Yaani iko hivi, kwa sababu umeshatangaza kwa watu kwamba wewe ni mwanachama mtiifu wa A, hata pale A inapokuwa na makosa, utafanya kila namna kuitetea, badala ya kutumia akili zako kufanya kilicho sahihi.
Je unawezaje kuondokana na itikadi?
Tukirudi kwa Charlie Munger anatushirikisha sheria aliyojiwekea ili asiingie kwenye itikadi. Munger anasema; I have what I call an iron prescription that helps me keep sane when I naturally drift toward preferring one ideology over another and that is: I say that I’m not entitled to have an opinion on this subject unless I can state the arguments against my position better than the people who support it. I think only when I’ve reached that state am I qualified to speak. This business of not drifting into extreme ideology is a very, very important thing in life.
Hapa anamaanisha; Nina kile ninakiita sheria ya chuma ambayo inanizuia kuegemea kwenye itikadi yoyote ile, sheria hiyo inasema; siruhusiwi kuwa na maoni juu ya jambo ambalo sina uwezo wa kutoa hoja dhidi ya msimamo wangu vizuri kuliko wale wanaokubaliana na jambo hilo. Ni pale tu ninapofikia kwenye hali hiyo ndipo ninastahili kuongea. Kutokujikita kwenye itikadi kali ni jambo muhimu sana kwenye maisha.
Hapa Munger ametupa suluhisho la uhakika la kutuzuia tusiingie kwenye itikadi kali. Anatuambia unapaswa kuelezea upande unaopingana nao vizuri kuliko unavyoweza kujielezea wenyewe. Kama wewe uko upande A na unapingana na upande B, inabidi uweze kuukosoa upande A ambao upo, kuliko anavyoweza kuukosoa aliyepo upande B. Pia inabidi uweze kuuelezea vizuri upande B unaoupunga, kuliko anavyoweza kuuelezea anayeukubali.
Hili linakulazimisha wewe ufikiri kwa kina na uache tu kufuata kundi. Na ukishafikiri kwa kina, utaona ni jinsi gani ilivyo ujinga kuingia kwenye itikadi yoyote ile. Kwa sababu ukiweza kukosoa upande wako kama anavyoweza kukosoa anayeupinga, na ukiweza kuuelezea vizuri upande unaoupinga kuliko yule anayeusimamia, utaona jinsi gani mambo ambayo watu wanabishania ni ya kijinga.
SOMA; Hiki Ndiyo Kitu Kimoja Kinachokutofautisha Na Viumbe Wengine Na Jinsi Ya Kukitumia Kwa Manufaa Yako.
Kuwa na utambulisho mdogo.
Mwanateknolojia na mwandishi wa Insha Paul Graham kwenye insha yake inayoitwa Keep Your Identity Small anaandika; I think what religion and politics have in common is that they become part of people’s identity, and people can never have a fruitful argument about something that’s part of their identity. By definition they’re partisan.
Akimaanisha dini na siasa vinafanana kwa kitu kimoja, huwa vinakuwa utambulisho wa mtu, na utambulisho unapohusika, watu hawawezi kuwa na mjadala wenye afya, wanaishia kuwa wanazi.
Kadiri unavyojitambulisha na makundi mengi, ndivyo itikadi yako inavyokuwa kali na inaathiri sana akili yako na maamuzi yako. Ukishajiambia na kuwaambia wengine kwamba mimi niko upande A, au mimi ni A wa kufa na kuzikwa, moja kwa moja umekataa upande B. Hivyo hata kama A ina mabaya yake, hutayaona, hata kama B ina mazuri yake hutayaona, wewe utasimamia A kwa nguvu zako zote, kitu ambacho hakina msaada kwako.
Hupaswi kuwa vuguvugu bali kutumia kinachofaa.
Ipo kauli moja ambayo watu huwa wanaitumia sana kutetea itikadi zao. Kauli hii inasema ni heri kuwa moto au baridi kuliko kuwa vuguvugu. Hivyo unapaswa kukubaliana na itikadi kama ilivyo, au kuipinga, hupaswi kuwa katikati.
Naweza kusema kauli hiyo ni mbovu kama itikadi nyingi zilivyo mbovu. Simaanishi kwamba uwe vuguvugu, bali namaanisha hupaswi kuganda kwenye upande mmoja.
Maji ya uvugu uvugu hayana manufaa kwako, kama majira ni ya joto, unahitaji maji baridi, na kama majira ni ya baridi unahitaji maji ya moto.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuziendea itikadi, usikazane na upande mmoja mpaka kufa, bali tumia kile chenye manufaa kutoka kwenye kila upande, kulingana na kile unachotaka kufanya.
Hakuna kitu kisichokuwa na matumizi kwenye maisha, hakuna kitu kisichokuwa na manufaa. Kila kitu kina ubaya na uzuri wake, kila kitu kina uimara na udhaifu wake na kila kitu kina faida na hasara zake.
Unachohitaji wewe kuangalia manufaa ya kitu yako wapi na kuyatumia na kujua madhara yako wapi na kuyaepuka. Usiende kama kuku aliyekatwa kichwa, kuwa kufanya kitu kwa sababu tu kila mtu anafanya au ndivyo umekuwa unafanya. Fungua akili yako, fikiri kwa kina na fanya maamuzi ambayo ni sahihi kwako kulingana na kile unachopitia.
Epuka sana itikadi kali, zina nguvu ya kuharibu akili yako na kuharibu kabisa maisha yako. Akili yako ina uwezo mkubwa mno, itumie kwa usahihi na utaweza kufanya makubwa.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania