Kwenye kilimo, kuna sheria ya Liebig ambayo inaeleza kwamba ukuaji wa mmea unategemea rasilimali yenye uhaba, na siyo upatikanaji wa rasilimali zote.
Kwa lugha rahisi ni kwamba, mmea utakua kulingana na upatikanaji wa rasilimali ambayo ina uhaba mkubwa. Hata kama rasilimali nyingine zote muhimu zinapatikana, ile yenye uhaba itazuia ukuaji kama haipatikani, na kuongeza ukuaji kama itapatikana.
Japokuwa sheria hii imekuwa inatumika sana kwenye kilimo, naona tunaweza pia kuitumia kwenye mafanikio yetu binafsi. Na hapa tunaweza kuona kwamba mafanikio yetu yanategemea sana ile rasilimali ambayo tunayo kwa uhaba.
Hata kama vitu vingine vyote vipo vya kutosha, kile muhimu ambacho una uhaba nacho, ndiyo kitakuwa kikwazo kwa mafanikio yako. Hivyo lazima uwe na mkakati wa kuhakikisha unaweza kuipata ile rasilimali ambayo una uhaba nayo zaidi.
Kwa mfano kama muda ni changamoto kwako, hicho ndiyo kitakuwa kikwazo kwa mafanikio yako. Hivyo itakuwa jambo la kushangaza, kama ukipata muda kidogo unaupoteza kwa mambo yasiyo muhimu. Ni sawa na upo jangwani, ambapo maji ni ya shida, halafu unapata maji kidogo unanawia miguu, wakati huna maji ya kunywa.
Kwa kuwa unajua mafanikio gani unayotaka kwenye maisha yako, orodhesha rasilimali zote unazohitaji kuwa nazo ili kuyafikia, kisha angalia ni rasilimali zipi una uhaba nazo mkubwa. Ukishazijua, weka mpango wa kuhakikisha unazitumia vizuri pale unapozipata.
Kwa wengi rasilimali zenye uhaba mkubwa ni muda, fedha, watu na hata utaalamu sahihi. Kwa kila rasilimali ambayo una uhaba nayo, jua ni kwa namna gani inakuwa kikwazo kwako kufanikiwa, kisha weka mkakati wa kuvuka kikwazo hicho.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,