Tumejifunza sana kuhusu umuhimu wa kuwa na orodha ya vitu ambavyo unapanga kufanya kwenye siku yako.
Orodha hiyo unaipanga kulingana na kipaumbele cha kitu, kisha unaifuata katika kuiendesha siku yako.
Hii ni nzuri na muhimu.
Lakini licha ya kuwa na orodha hii, bado kuna mambo huwa yananyemelea na kuchukua muda wetu ambayo tunapaswa kuyadhibiti kama tunataka kuwa na uzalishaji mzuri.
Na hapa ndipo unapohitaji orodha ya aina nyingine, orodha ya vitu ambavyo hutavifanya kwenye siku yako.
Kuandaa orodha hii, angalia vitu ambavyo unapenda kufanya kila siku, lakini havina mchango wowote kwenye kile unachotaka kupata au unakotaka kufika. Kisha orodhesha vitu hivyo na jiambie kwamba hutavifanya kwenye siku yako.
Unapoandika chini na kujiambia kwamba hutafanya, inakuwa na nguvu kuliko kutokuweka nia ya aina hii.
Ni vizuri pia kuiweka orodha hiyo kwenye eneo ambalo utaiona mara kwa mara ili kuhakikisha hupotezi muda wako kwenye mambo yasiyokuwa muhimu kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,