Kama fedha ilivyokuwa muhimu katika mahusiano yetu vivyo hivyo na msamaha ulivyokuwa muhimu katika mahusiano yetu. Ni mara ngapi tunakwazana katika mahusiano yetu? vuta picha kama mahusiano yetu yasingekuwa na msamaha maisha yanguwaje?

Tunakoseana kwa mengi, na hakuna mtu ambaye ni mkamilifu hivyo kitu kinachorudisha mahusiano yetu pale yanapovunjika ni msamaha wa kweli tu. Ni nani ambaye hajawahi kupishana kauli katika mahusiano yake? Iwe ni ya kindugu, kifamilia,kikazi nk. Kuna wakati kweli tunateleza lakini inafikia mahali tunaamua kuachilia uchungu wote na kurudisha mahusiano yetu ya awali kwa njia ya msamaha wa kweli.

Ni kujidanganya pale unaposema unaweza kuishi bila kuhusiana na watu, ni uongo huwezi kuishi bila kuwa na mahusiano na wengine. Sisi binadamu ni viumbe ambavyo tumezaliwa na mahusiano ya vinasaba yaani DNA kwa vyovyote vile huwezi kukwepa mahusiano.

Kwa utangulizi huo hapo juu umeshapata picha kuwa ni namna gani msamaha  ulivyo muhimu katika maisha yetu.

Swali la kujiuliza hapa je tunasamehe kwa faida ya nani?

Watu wengi huwa wanafikiri tunasamehe kwa sababu ya watu wengine, jibu sahihi ni kwamba tunasamehe kwa faida yetu sisi wenyewe ili mambo yetu yaende.

Kwa sababu, kutokusamehe ni kuendelea kujitesa wewe mwenyewe wakati aliyekukosea akiendelea na maisha yake wewe unaendelea kuvumilia uchungu huku ukiendelea kukutafuna taratibu.

Unapaswa kujua hilo kwamba unaposamehe unasamehe kwa faida yako mwenyewe na siyo kwa ajili ya mtu mwingine.

SOMA; Huu Ndiyo Aina Ya Msamaha Usiyo Kuwa Na Fadhila

Hasara moja wapo ya kutokusamehe ni kuruhusu adui yako aendelee kukutawala kiakili, badala ya wewe kufikiria mambo muhimu unakuwa unamfikiria adui yako. Wakati huo huo wewe ukiendelea kumfikiria adui yako yeye akiendelea kufanya yake wewe unaendelea kuteseka.

Tunaalikwa kuachilia maumivu tuliyonayo, tuwasamehe wale waliotuudhi kwani tusiposamehe tunaendelea kuumia na kumbuka kuwa msamaha siyo kuvumilia bali msamaha ni kuondoa uchungu ulioumbika ndani ya moyo.

Hatua ya kuchukua leo; una samehe kwa faida yako mwenyewe, hivyo samehe ili maisha yako yaende na kumbuka unapokataa kusamehe unaruhusu adui yako aendelee kutawala akili yako.

Kwahiyo, wakati mwingine unapaswa kusamehe wewe mwenyewe, hata kama wewe siyo mwenye kosa, samehe na endelea na maisha yako usimsubiri mpaka yule aliyekukosea ndiyo aje akuombe msamaha. Ni rahisi sana kumwekea adui yako kaa la moto kichwani kwa kumsamehe kosa ambalo hakutegemea kusamehewa.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa http://kessydeo.home.blog ,vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana