Unazaliwa na kipaji, unajifunza ujuzi.
Hivi ni vitu viwili muhimu sana unavyohitaji kwenye safari yako ya mafanikio.
Kuna wale wanaozaliwa na vipaji, na kufikiri hivyo pekee vinawatosha bila ujuzi, hawa huwa wanashindwa na wenye ujuzi ila wasio na kipaji kama chao.
Na kuna wale ambao wanazika vipaji vyao na kukazana na ujuzi, hawa huweza kupiga hatua kubwa, lakini maisha yao yanakuwa hayajakamilika, kwa sababu kile kikubwa ndani yao wanakuwa hawajakitumia.
Utapata mafanikio makubwa na kuridhika na maisha yako kama utajua kipaji chako na kisha kujenga ujuzi kwenye kipaji hicho. Hapo utakuwa tayari kujituma sana kwa sababu hutakuwa unafanya kazi, bali kile unachopenda kufanya.
Usidanganyike na kipaji au uwezo fulani mkubwa ulionao, badala yake jenga ujuzi kwenye kipaji na uwezo ulionao, kisha weka juhudi kubwa kwenye kufanya kazi na utaweza kupiga hatua kubwa sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,