Kabla hujafanikiwa, unaamini kwamba mafanikio ni kujumlisha, yaani kuwa na vitu vingi zaidi, hivyo unapambana ili kupata vingi uwezavyo.

Unapofanikiwa, unagundua kwamba mafanikio ni kutoa, yaani kuwa na vitu vichache ambavyo ni muhimu, unavithamini kweli na vina maana kubwa kwako.

Kabla hujafanikiwa unaamini unapaswa kufanya kila kazi au biashara inayokuja mbele yako na unaweza kuifanya. Hivyo unajikuta ukisumbuka na mambo mengi. Kweli yanakupa faida, lakini kadiri unavyofanikiwa unagundua nguvu nyingi unazipoteza kwa mambo yasiyo sahihi, ambapo kama utaacha kuzipoteza kwenye mambo mengi na kupeleka nguvu hizo kwenye mambo machache muhimu, utaweza kufanya makubwa zaidi.

Kabla hujafanikiwa unaamini unapaswa kujifunza kila kitu, kumsikiliza kila mtu na kusoma kila aina ya kitabu. Hivyo unakuwa wazi kujifunza kila aina ya maarifa unayokutana nayo. Kadiri unavyofanikiwa unagundua kwamba maarifa mengi unayoyapata yanakinzana, wakati kwenye eneo moja unajifunza kitu fulani ni salama, kwenye eneo jingine unajifunza kitu hicho ni hatari. Hapa ndipo unajifunza umuhimu wa kuchagua aina ya maarifa utakayofuatilia na aina ya watu utakaojifunza kwao, ambao ni wachache na watakufikisha kule unakotaka kufika.

Kiwango cha juu kabisa cha mafanikio ni ubobezi kwenye yale machache na muhimu. Hivyo kuweza kuyajua machache na muhimu kwako na kupuuza mengine yote ni hatua muhimu sana kuchukua kwenye maisha yako. Kadiri unavyopata utambuzi huu mapema, ndivyo unavyopunguza ugumu wa safari yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha