James Stockdale (December 23, 1923 – July 5, 2005) alikuwa mwanajeshi wa anga wa Marekani ambaye alipewa tuzo ya heshima kwenye vita ya Vietnam ambapo alikamatwa na kushikiliwa kama mfungwa wa kivita kwa zaidi ya miaka saba.

Baada ya kukamatwa, James alipitia mateso makali mno katika kipindi cha ufungwa wake wa kisiasi nchini Vietnam. Kuna kipindi alilazimika kujiumiza usoni kwa makusudi ili kuepuka kutumiwa na Wavietnam katika propaganda zao kwenye vita hiyo.

Pamoja na kupitia magumu hayo kwa miaka hiyo zaidi ya 7, James aliweza kuwa imara na hatimaye kuweza kurudi katika uhuru wake baada ya kuokolewa kwenye ufungwa ambao alikuwa ametekwa.

Mwandishi Jim Collins wakati anafanya utafiti wake wa kitabu cha Good To Great alifanya mahojiano na Stockdale. Katika mahojiano hayo Collins alimuuliza ni kitu gani kilimwezesha kuvuka miaka hiyo ya mateso makali.

stockdale 1

Stockdale alijibu: “Sikuwahi kuwa na wasiwasi kuhusu kutoka kwangu, niliamini nitavuka kipindi hicho kigumu na kutumia uzoefu nilioupata kama tukio litakalobadili kabisa maisha yangu, tukio ambalo siwezi kubadilishana na yeyote kwa gharama yoyote ile.”

Maelfu ya wanajeshi walikamatwa pamoja na Stockdale na kufungwa gereza moja, lakini ni wachache walioweza kupona, wengi walikufa kabla ya kuokolewa. Collins alimuuliza Stockdale ni watu wa aina gani ambao walikufa mapema.

Stockdale alijibu: “Ni wale wenye matumaini hewa. Wale waliokuwa wanasema, tutatoka kabla ya Krismasi, halafu Krismasi inakuja na inapita, wanasema tutatoka kabla ya Pasaka, halafu pasaka inakuna na inapita. Wanasema tena tutatoka kabla ya Krismasi, na waliendelea na matumaini hayo mpaka walipokufa wakiwa wamevunjika mioyo.”

Kupitia mahojiano haya, Stockdale anatufundisha kitu kimoja muhimu sana; tunapaswa kuamini kwamba tutavuka chochote tunachopitia, lakini tunapaswa kuepuka sana kuwa na matumaini hewa.

Kilichowafanya wengi kufa mapema ni kushindwa kukabili uhalisia ambao haukuwa mzuri kwao. Waliamua kutumia mbinu ya mbuni kufukia kichwa chake kwenye mchanga ili asiione hatari, kwa kutokujua kwamba kuchagua kutokuiangalia hatari hakuifanyi iondoke. Mbinu hii inamsaidia mtu asikabiliane na ukweli mchungu, lakini haiwezi kufanya kazi kwa muda mrefu, kadiri muda unavyokwenda na mambo kutokuwa kama mtu anavyotegemea, anakata tamaa na kufa au kuanguka.

Stockdale alikabiliana na ugumu kwa njia na mtazamo wa tofauti. Alikubaliana na uhalisia wa hali ilivyo, alijua kabisa kwamba kipindi atakachopitia ni kigumu mno na hivyo alichukua hatua sahihi za kuhakikisha hakati tamaa katika kipindi hicho. Kwa kujua hali itakuwa ngumu na kutokujidanganya, kulimfanya aweze kukabiliana na ukweli na kujenga imani yake kwamba hilo litaputa, japo hakujua ni lini.

SOMA; Kitu Hiki Kimoja Kitakufanya Ufe Kabla Ya Wakati Wako.

Jinsi Ya Kukabiliana Na Mlipuko Wa Virusi Vya Corona Unaoendelea.

Mlipuko wa virusi vya Corona unaoendelea sasa duniani, unaibadili kabisa dunia. Kila mtu ameathirika kwa namna fulani na virusi hivi. Virusi hivi vimeleta madhara makubwa matatu, kiafya kwa watu kufa, kiuchumi kwa watu kupoteza kazi na biashara na kijamii kwa mfumo wa maisha kubadilika kabisa.

Ubaya wa mlipuko huu ni kwamba hakuna anayejua utaisha lini na mambo kurudi vizuri lini. Kuna matarajio mbalimbali yanayowekwa na wataalamu mbalimbali. Wapo wanaosema itachukua miezi mitatu, wengine miezi 6 na wengine mwaka.

Watu wengi wamekuwa wanajipa matumaini hewa kwamba baada ya muda mfupi, mlipuko huu utakua umeisha na mambo yatarudi sawa. Na hapa ndipo wengi wanajiandaa kufa mapema, kwa sababu hakuna anayejua lini mlipuko huu utaondoka kabisa. Baadhi ya nchi ambazo zilikuwa zimetangaza hakuna tena maambukizi mapya, zimeanza kupata maambukizi mapya, hii ikionesha kwamba mambo siyo rahisi kama tunavyofikiri.

Stockdale 2

Hivyo kupitia Stockdale tunajifunza njia sahihi ya kukabiliana na mlipuko huu wa virusi vya Corona, ili tuweze kuvuka salama na maisha yetu kwenda vizuri. Kwa majibu mawili ambayo Stockdale aliyatoa kwa Collins, tunaifunza hatua mbili za kuchukua juu ya hili;

Moja; amini hili litapita.

Hatua ya kwanza na muhimu kabisa kwako kuchukua ni kuamini kwamba mlipuko huu utapita. Na usiishie hapo, bali amini kwamba mlipuko huu utapita na kukuacha wewe ukiwa salama kabisa. Pamoja na magumu mengi utakayopitia kwenye hali hii, usikubali kupoteza imani hii kwa namna yoyote ile. Tuna mifano mingi ya dunia kupitia mambo magumu na ikavuka, hivyo hili pia tutavuka.

Mbili; achana na matumaini hewa.

Baada ya kuamini kwamba hili litapita na kukuacha salama, unapaswa kuachana na matumaini hewa. Unapaswa kuukabili ukweli kama ulivyo na siyo kujidanganya. Usijiaminishe chochote ambacho huna uhakika au ushahidi nacho.

Na hapa ndipo pa kuwa makini sana na lini hali hii itaisha. Ukweli ni kwamba hakuna anayejua, kila anayetabiri ni kubashiri tu, hakuna anayejua. Inaweza kuchukua miezi mitatu, au sita, au mwaka au zaidi ya hapo.

Kilicho muhimu kwako ni kuwa tayari kukabiliana na uhalisia wa hali hii. Kwamba mambo yatakuwa magumu, uchumi utaathirika, mfumo wa afya utatikiswa na hali za kijamii zitabadilika sana.

Wajibu wako ni kuhakikisha kila siku unaikabili kama inavyokuja kwako na kuhakikisha hupotezi imani kwamba tutavuka hili. Kuhakikisha unaendelea kuwa salama kiafya na kujiimarisha kiuchumi pamoja na kujiboresha kijamii ili uweze kuvuka hili salama.

Hivyo ndivyo tunaweza kuvuka wakati huu mgumu tunaopitia sasa, kwa kuamini tutauvuka huku tukiachana na matumaini hewa kwa kukabiliana na ukweli kama ulivyo.

Nikukaribishe sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA kama bado hujawa mwanachama, kwa sababu kwenye KISIMA CHA MAARIFA tunajenga jamii ya tofauti kabisa, jamii inayoishi kwa misingi hii miwili, kuamini tunaweza kufanya makubwa lakini kutokujidanganya kwamba mambo ni rahisi. Hakuna sehemu inaweza kukupa amani katika kipindi hiki kama KISIMA CHA MAARIFA. Karibu sana tuvuke pamoja katika kipindi hiki ambapo kila mtu anataka tamaa na kuona mambo hayawezekani. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwenda wasap namba 0717396253 na utapewa maelekezo. Karibu sana.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania