Maisha ni sawa na kusukuma jiwe kwenda juu ya mlima.

Ukisukuma linaenda, ukiacha kusukuma linarudi chini.

Kama unatafuta njia ya kumaliza matatizo yote kwenye maisha yako rafiki yangu, unajidanganya, haipo njia hiyo, wala hakuna mwenye uwezo huo.

Mwisho wa matatizo yako yote ni pale utakapokufa.

Kadiri unavyokuwa hai, matatizo hayatakosekana.

Unakutana na tatizo moja, unalitatua, ule utatuzi wako unazaa tatizo jingine, na hali inaendelea hivyo.

Una changamoto ya kipato, unaamua kuanzisha biashara ambayo itaongeza kipato chako, kweli biashara hiyo inaongeza kipato, lakini inakuja na matatizo yake mengi, kujihusisha na watu mbalimbali ambao wanakuumiza kichwa na kukukosesha usingizi.

Wakati mwingine utatuzi uliofanya kazi siku za nyuma, unashindwa kuendelea kufanya kazi, hivyo inabidi uje na utatuzi mpya.

Hakuna siku maisha yatakuwa vile unavyotaka kwa kila eneo la maisha yako, utakuwa na matatizo na changamoto mbalimbali, utakutana na magumu. Unavuka ugumu mmoja, unakutana na ugumu mwingine mkubwa zaidi.

Njia bora ya kwenda na haya maisha ni kuishi siku moja kwa wakati, kutatua tatizo moja kwa wakati, na ukimaliza hilo, jua kuna jingine linakusubiri. Ukabili uhalisia na usijidanganye kwa namna yoyote ile.

Asili ina njia mbalimbali za kukujaribu kama kweli umeiva kabla haijakupa mafanikio, na hata ikishakupa mafanikio, huwa na mbinu mbalimbali za kujaribu kukunyang’anya mafanikio yako.

Kila siku unayoamka jua ni siku ya mapambano, siyo lele mama, ni kazi kweli. Lakini nafasi ya kushinda ni kubwa, ila ukishashinda siyo mwisho, bali mwanzo wa mapambano mengine makubwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha