Tumeshajifunza sana kuhusu kujua wapi unataka kufika na maisha yako, kuwa na mpango kamili wa jinsi ya kufika kule unakotaka kufika.
Lakini pamoja na wengi kujua wapi wanataka kufika, pamoja na kuwa na mpango kamili wa kufika huko, bado ni wachache sana wanaofika wanakotaka kufika.
Wengi wana kila aina ya sababu, wanasubiri mpaka wapate hiki, au wanasubiri kile kipite na sababu nyingine kama hizi.
Kabla sababu moja haijaisha, nyingine inaibuka, ukija kustuka miaka imepita na hujafanya ulichokuwa umepanga.
Suluhisho la tatizo hili ni moja, kuamua mara moja kwamba unaanzia wapi. Pamoja na mipango mikubwa uliyonayo, kama hutaamua mara moja unakwenda kuanzia wapi, hutakwenda kuanza.
Niamini kwenye hilo, kama utaendelea kujiambia unasubiri vitu fulani ndiyo uanze, utasubiri mno, maana sababu za kusubiri huwa haziishi.
Jiambie kabisa unakwenda kuanzia wapi na unaanza lini, kisha anza kweli, na hapo ndipo utaweza kufika kule unakotaka.
Huhitaji kuanzia juu sana, huhitaji kufanya makubwa sana, unachohitaji ni kuamua wapi unakwenda kuanzia na kuanza.
Kuanza ndiyo jawabu la yote, na ukishaanza, hakikisha huachi, hata iweje, nenda na kanuni ya mwendo, piga hatua kila siku, ishi siku moja kwa wakati na usiahirishe chochote.
Ugumu mkuu kwenye mafanikio ni subira, wengi wanakosa hilo na ndiyo maana pamoja na kujua wanachotaka na kuwa na mpango wa kupata wanachotaka hawakipati.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha, haijalishi naanzia wapi? Mpango mzima ni subira na kuendelea kuchukua hatua kila siku na hapa mafanikio ni uhakika.Tupo pamoja.
LikeLike