Ili kupata mafanikio makubwa, unapaswa kufikia ubora wa kutisha na siyo ubora wa kutosha.

Ubora wa kutosha ni pale unapoweza kufanya kile unachofanya vizuri kuliko wengine, lakini watu wanaweza kuficha ubora wako huo na usipate ushindi.

Ubora wa kutisha ni pale unapoweza kufanya kile unachofanya vizuri sana kuliko wengine, kiasi kwamba hakuna anayeweza kuficha ubora wako, hivyo hakuna anayeweza kukuzuia usipate ushindi.

Mwandishi Carl Newport anaita ubora wa kutosha SO GOOD THE CAN’T IGNORE YOU, kwenye kitabu chake kinachokwenda kwa jina hilo. Anachomaanisha ni unakuwa bora sana kiasi kwamba hakuna anayeweza kukupuuza. Hata wale ambao hawakubaliani na wewe, hawana jinsi ila kuja kwako kunufaika na unachofanya au unachotoa.

Charlie Munger huwa ana msimamo huu, kama jambo lina hatari kwenye mita 5, basi yeye anachukua tahadhari ya mita 50, hivyo hatari kwake inakuwa ndogo zaidi. Hiki ni kitu kile kile, kuwa bora sana kiasi kwamba hata bahati mbaya haiwezi kukugusa.

Rafiki, kama unataka kupoteza muda wako na nguvu zako kuwalaumu wengine, kuwa na ubora wa kutosha, maana utawapa nafasi ya kuficha au kukwamisha ubora huo kwa manufaa yao binafsi.

Lakini kama unataka yeyote aiseze kukuzuia, basi kuwa na ubora wa kutisha, ubora wa hali ya juu sana kiasi kwamba hakuna anayeweza kuuficha au kuupuuza, inakuwa wazi kwamba anayetaka kile kinachohusiana na wewe, basi anakuja kwako.

Ni rahisi kumlalamikia refa kwamba amependelea timu pinzani ndiyo maana timu yako ikashindwa, lakini kama timu yako ingeweka juhudi kubwa na kuwa na ubora wa kutisha, hata refa angefanya nini, timu hiyo ingeshinda tu.

Ni rahisi kulalamikia hali ya uchumi pale biashara yako inapokwenda vibaya, lakini kama ungeweka juhudi kubwa kuijenga biashara hiyo kwa namna ambayo haiwezi kuathiriwa na mabadiliko yoyote, ingeweza kuvuka hali yoyote inayopitia.

Kumbuka hili rafiki, ni ubora wa kutisha na siyo wa kutosha. Ongeza juhudi ili kufikia ubora huo wa kutisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha