Kipindi cha nyuma, kabla ya kuingia kwenye hizi zama za taarifa, wazo la biashara lilikuwa kitu kizito sana.

Wazo la biashara lilikuwa na thamani kubwa sana na watu walifanya mawazo yao ya biashara kuwa siri na kuyalinda kwa gharama kubwa.

Lakini tangu tumeingia kwenye zama za taarifa, taarifa zimekuwa zinasambaa kwa kasi na mawazo ya biashara yamekuwa mengi na hakuna siri tena.

Kila mtu anaweza kujua muundo wa biashara yoyote ile inayofanyika, na anaweza kujifunza na kuanzisha biashara yoyote ile kama inavyofanywa na wengine.

Hivyo kwa sasa kinachowatofautisha wanaofanikiwa kwenye biashara na wanaoshindwa siyo wazo, bali juhudi ambazo mtu anaweka.

Kama kuna biashara mbili, ambazo ni za wazo moja na ziko eneo moja, biashara itakayoshinda ni ile ambayo kunawekwa juhudi kubwa zaidi.

Juhudi za kuongeza wateja na kuwashawishi kununua zaidi, juhudi za kupunguza matumizi, juhudi za kuwapata watu sahihi na mengine.

Hakuna biashara inayoweza kusimama na kufanikiwa kwa sababu tu ina wazo bora. Kila biashara inayosimama imara na kufanikiwa, ni matokeo ya juhudi kubwa ambazo zimewekwa na kwa muda mrefu.

Hivyo basi, katika zama tunazoishi sasa, thamani ya wazo la biashara ni sawa na bure. Thamani kubwa ipo kwenye juhudi zinazowekwa.

Hivyo mfanyabiashara au mjasiriamali ambaye atakuwa tayari kujitoa kwelikweli kukuza biashara yake, kwa kuweka kazi bila ya kuchoka, kuendelea kuchukua hatua bila ya kukata tamaa pale anaposhindwa, ndiye atakayefikia mafanikio makubwa.

Hakuna kinachoweza kukuzuia wewe kwenye hilo, hata kama huna uwezo wa kuja na wazo bora na la kipekee, anza na wazo lolote lililopo, kisha fanya kwa ubora zaidi ya wengine wanavyofanya.

Kama wewe au mtu mwingine anakuambia kwamba hajaanza biashara kwa sababu hajapata wazo la biashara, jua wazi hicho ni kisingizio tu, ukweli ni kwamba wewe au mtu huyo bado hajawa tayari kuweka juhudi ili kuanzisha na kufanikiwa kwenye biashara. Hivyo anajificha kwenye wazo, kitu ambacho thamani yake ni ndogo mno kwenye biashara kwenye zama hizi.

Nenda kaweke juhudi, hizo tu ndiyo zitakutofautisha na wengine, na siyo wazo ambalo kila mtu anaweza kuliiga. Ni wachache sana ambao wako tayari kuweka juhudi kubwa, hivyo ukitumia njia hii, utafanya makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha