Kama unataka kufanikiwa, lazima uijue saikolojia ya binadamu. Bila ya ujuzi huu muhimu, utakwama kwenye mambo mengi mno.

Moja ya vitu vya kujua kuhusu saikolojia ya binadamu ni wivu. Pale unapofanya jambo jipya na kubwa ambalo wengine hawajawahi kufanya, wataingiwa na wivu.

Hivyo watafanya kila namna kuhakikisha huendelei kufanya au unashindwa kwenye hicho unachofanya. Na ili kukukwamisha, wanaangalia udhaifu wako uko wapi na kutumia huo kukukwaisha au kukuangusha.

Udhaifu ambao ni rahisi kwa kila mtu kuutumia ni kutokujiamini. Ukishaonesha dalili za kutokujiamini, basi umekwisha, watu watatumia udhaifu huo kuhakikisha wanakuangusha.

Kutokujiamini kunaonekana wazi pale unaposema unajaribu kufanya kitu. Watu wakishajua unajaribu, basi wanahakikisha wanazuia jaribio hilo lisifanikiwe.

Hivyo hatua muhimu ya wewe kuchukua ni kuhakikisha huonekani kama unajaribu kitu. Kuhakikisha unaonekana unajiamini hata kama ndani yako una wasiwasi. Usioneshe wasiwasi wowote kwa nje.

Watu huwa wanawaamini wale ambao tayari wanajiamini. Ndiyo maana wanasiasa huwa wanapata wafuasi, kwa sababu hata kama wanadanganya, wanafanya hivyo kwa kujiamini. Hakuna mwanasiasa anayesema kitu bila ya kujiamini. Hivyo pamoja na kwamba tunajua kabisa wanatudanganya, kile kitendo cha kujiamini kinatufanya na sisi tuwaamini.

Unapaswa kutumia udhaifu huo uliopo kwenye saikolojia ya wanadamu kuhakikisha hawakuzuii kupiga hatua unazotaka kupiga. Jiamini, yaani usitetereke kwa namna yoyote ile. Hata kama ndani yako una hofu kubwa, nje usoneshe dalili zozote. Mtu anapokuja kwako kwa lengo la kukukwamisha au kukukatisha tamaa, onesha kwamba unajiamini na una uhakika wa kupata unachotaka, na utashangaa ghafla mtu huyo anabadilika na kukuamini.

Kujiamini ndiyo njia pekee itakayowazuia watu wasikukwamishe kwenye mipango yako. Itumie kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha