Fikiria umejipanga kufuatilia taarifa ya habari ya siku ili kujua yale yanayoendelea. Muda unafika na kuwasha tv au redio yako tayari kwa ajili ya kupata habari. Mtangazaji anakuja na kusema; ndugu watazamaji/wasikilizaji tunasikitika kuwaambia kwamba leo hakuna habari yoyote, hivyo mnaweza kuendelea na mambo mengine.

Hujawahi kusikia hivyo, na wala hutakuja kusikia kauli kama hiyo maisha yako yote. Hii ni kwa sababu kazi kuu ya vyombo vya habari ni kutangaza habari, na kama hakuna habari za kutangaza, basi vinatengeneza habari na kuzitangaza.

fake_news_burning_newspaper.jpg

Mimi huwa siyo mfuatiliaji wa habari za aina yoyote ile. Tangu dunia imekumbwa na mlipuko wa virusi vya Corona, vitu vingi sana vimesimama, na moja ya vitu ambavyo vimesimamishwa kabisa ni michezo ya kila aina. Hili lilinifanya kufikiria kama michezo yote imeahirishwa dunia nzima, vipindi vya michezo vitakuwa havina kitu cha kutangaza na hivyo hakutakuwa tena na habari za michezo?

Basi kupima hilo siku moja nikasema wacha nisikilize habari za michezo kwenye redio yoyote ile. Nikafungulia redio na kusikia kipindi cha michezo kinaendelea kama kawaida. Nikataka kujua ni habari gani muhimu ya michezo inayopatikana wakati ambapo michezo yote duniani imesimamishwa. Na hii ndiyo ilikuwa habari kuu; wachezaji washauriwa wasile chipsi wakati huu ambapo michezo imesimamishwa.

Nilishangaa sana hizi kuwa ndiyo habari, kwa sababu hayo ni mambo ya msingi kabisa ambayo kila mchezaji anapaswa kuyajua, kuhusu ulaji na ufanyaji wa mazoezi. Wakati ambapo michezo inaendelea huwezi kusikia habari kama hizo. Ila kwa kuwa hakuna bahari za michezo inayoendelea, basi waandishi wanafanya kile ambacho ni wajibu wao kufanya, kutengeneza habari.

Mtu mmoja amewahi kusema kazi ya vyombo vya habari ni kutafuta habari za kuweka katikati ya matangazo. Yaani lengo la kwanza la chombo chochote cha habari ni kurusha matangazo, maana hayo ndiyo yanaingizia chombo hicho fedha. Sasa kwa kuwa chombo hakiwezi kurusha matangazo kwa masaa 24, kinatafuta vitu vya kusisimua ambavyo itaweka katikati ya matangazo, ili uendelee kufuatilia chombo hicho.

SOMA; Ufafanuzi Wa 20 Kwa 20; Mitandao Ya Kijamii, Habari Na Ushauri.

Ni sherehe kwa vyombo vya habari.

Kwa hali inayoendelea sasa ya mlipuko wa virusi vya Corona, kwa vyombo vya habari ni sherehe. Sasa ndiyo wakati wa vyombo vya habari kuhakikisha vinapata wafuatiliaji wengi viwezavyo. Kwa sababu watu wana kiu ya kujua kila kinachoendelea, kwa kila dakika. Na kwa kuwa shughuli nyingi zimesimama au kupungua, watu wana muda zaidi wa kufuatilia habari.

Sasa unafikiri chombo cha habari kitafanya nini katika hali kama hii, kama hakuna habari muhimu kutangaza? Lazima habari zitengenezwe, kwa namna ambayo zinawasisimua watu na kuwafanya waendelee kufuatilia chombo hicho.

Wito wangu kwako ni ule ule.

Rafiki yangu mpendwa, wito wangu kwako ni ule ule wa siku zote, achana na habari, usiwe mfuatiliaji wa habari, hakuna chochote unachojifunza kwenye habari zaidi ya kupata msisimko wa akili na kujawa hofu kwamba dunia imefika mwisho.

Lakini utaniuliza sasa nitajuaje kuhusu mambo yanayoendelea hasa wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona? Na jibu liko wazi, fuatilia vyanzo vya uhakika vinavyotoa taarifa sahihi kuhusu hali hiyo ya ugonjwa.

Usifuatilie kila habari kuhusu hali hii, nyingi ni hasi na zina lengo la kukujaza wewe hofu. Epuka sana habari za mitandaoni katika kipindi hiki, kila mtu anaweza kuchagua kusema chochote, hata kama siyo sahihi au kweli.

Na kama kuna jambo muhimu sana ambalo unapaswa kulijua, ambalo linatoka kwenye habari, basi kuna watu watakuambia. Hivyo usipoteze muda wako kwenye habari.

Kama ambavyo Altucher anatuambia kwenye nukuu hapo chini, lengo la habari ni kupata wafuatiliaji, iwe ni kwa kudanganya au kudhalilisha wengine. Usiwe mteja wa vitu hivyo.

“Never read news. The news is written by bad writers who are just looking for page views and are willing to lie or defame to get them. Also the news is out of date one day later.” – James Altucher

Hakuna unachojifunza kwenye habari.

Habari hazijawahi kuwa na lengo la kumfundisha mtu kitu chochote kile, lengo la habari ni kutoa taarifa, taarifa ambazo wewe unayesikiliza huna hata cha kufanya.

Fikiria taarifa ya habari inayokueleza kuhusu ajali iliyotokea eneo la mbali. Umejifunza nini kwenye taarifa kama hiyo? Hakuna. Unaweza kusema labda kuna ndugu yako yuko kwenye ajali hiyo, lakini je unafikiri kama ndugu yako amefariki kwenye ajali utasubiri kusikia kwenye habari?

Kama ambavyo Jefferson anatuambia kwenye nukuu hapo chini, kusoma habari pekee unakuwa mjinga kuliko yule ambaye hasomi chochote. Kwa kifupi kufuatilia sana habari kunakufanya uwe mjinga zaidi.

“I do not take a single newspaper, nor read one a month, and I feel myself infinitely happier for it. The man who reads nothing at all is better informed than the man who reads nothing but newspapers.” ~ Thomas Jefferson

Tumia muda wako kusoma vitabu.

Ukiacha kufuatilia habari ambazo hazina chochote cha kukufundisha, utapata muda mwingi sana ambao unaweza kuutumia kusoma vitabu na ukapata maarifa yatakayokusaidia sana.

Habari nyingi unazofuatilia zina matumizi ya muda mfupi sana, yaani zinaisha muda wake baada ya siku kupita. Lakini unaposoma vitabu, unapata maarifa ambayo hayapitwi na wakati, unaweza kuyatumia muda wowote wa maisha yako.

Hivyo achana na habari na tumia muda huo kusoma vitabu, kujiongeza maarifa ambayo yatakuwezesha kufanya maamuzi bora kwenye maisha yako.

Kama ambavyo Taleb anatuambia kwenye nukuu hapo chini, kama unasubiri ujifunze kitu kupitia habari umeshachelewa, njia pekee ya kujifunza ni kusoma vitabu, hivyo achana na habari na upate muda wa kusoma vitabu.

Public information can be useless, particularly to a businessman, since prices can already “include” all such information, and news shared with millions gives you no real advantage. Odds are that one or more of the hundreds of millions of other readers of such information will already have bought the security, thus pushing up the price. I then completely gave up reading newspapers and watching television, which freed up a considerable amount of time (say one hour or more per day, enough time to read more than a hundred additional books per year, which, after a couple of decades, starts mounting). – Nassim Taleb

SOMA; Pata Zawadi Ya Vitabu Nane (08) Vya Maendeleo Binafsi Na Mafanikio Kwenye Kazi, Biashara Na Maisha Kwa Ujumla.

Rafiki yangu mpendwa, kwa kuwa hakuna siku chombo cha habari kitakuambia leo hakuna habari, basi wewe ndiye mwenye nguvu ya kukiambia chombo cha habari leo sitaki habari zako, nimechoshwa na hofu unazonijengea kila siku na natumia muda wangu kusoma vitabu ili nipate maarifa zaidi.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania