Kipindi cha nyuma, ajira hasa za serikalini zilionekana ndiyo usalama pekee wa kipato ambao mtu anaweza kuwa nao.

Mtu alikuwa akipata ajira serikalini, ilikuwa ni uhakika mpaka siku anakufa. Hivyo kupata ajira hizo ilikuwa ni tiketi ya kuwa na uhakika wa kipato mpaka siku unakufa.

Lakini kwa sasa hali haipo hivyo, ajira zote hazina tena usalama wa aina hiyo, tunaona hata wale walio na ajira za serikalini wakizipoteza kwa makosa ambayo siyo yao.

Na hata wale ambao hawapotezi ajira hizi, zimekuwa mzigo kwao badala ya kuwasaidia. Mazingira ya kazi yanakuwa magumu na ya hofu, huku kukiwa hakuna ongezeko la mshahara linaloweza kuendana na kupanda kwa gharama za maisha.

Hivyo basi, kutokana na kile kilichotegemewa sana kubadilika, ni lazima kila mtu abadilike pia.

Kwa sasa usalama pekee ulionao kwenye upande wa kipato ni uwezo wako wa kulipwa. Yaani una uwezo kiasi gani wa kuwashawishi watu wakulipe kwa bidhaa au huduma unazoweza kuwapa na zikaongeza thamani kwenye maisha yao.

Kadiri unavyokuwa na uwezo mkubwa kwenye hilo, ndivyo unavyokuwa huru kifedha.

Uwezo wako wa kulipwa unaendana sana na uwezo wako wa kuuza. Na hapo ni kuwa na bidhaa au huduma ambayo inaongeza thamani kwa wengine, na kuweza kuwashawishi wainunue.

Kila siku kazana kuwa bora kwenye eneo hili la kuingiza kipato, hasa kupitia mauzo. Haijalishi unafanya kazi gani sasa, hakikisha kuna kitu ambacho wewe unakiuza nje ya kazi hiyo. Weka juhudi kutengeneza wateja ambao wanakuamini na kukutegemea kwa kile unachouza na wapo tayari kununua kwako pale wanapokuwa na uhitaji.

Kila siku jifunze jinsi ya kuwa muuzaji bora zaidi, jinsi ya kuwa na ushawishi na jinsi ya kuongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine. Fanyia kazi hayo unayojifunza na ona kipato chako kikiongezeka. Unapoona kipato kikiongezeka, unajiamini zaidi na kuwa huru zaidi.

Ajira hata kama umeambiwa ni ya milele na inakulipa kiasi kikubwa cha fedha, usibweteke, uwezo wako wa kuingiza kipato wewe mwenyewe kupitia kuuza ndiyo kitu unachoweza kutegemea maisha yako yote na kisikuangushe.

Hata pale uchumi unapoyumba, bado wewe utakuwa na uwezo wa kuuza, hata kama ajira yako itafikia ukomo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha