Utakuwa na maisha rahisi kama utaacha kupokea ushauri ambao watu wengi wanakupa, hata kabla hujawaomba.

Na utakuwa na maisha tulivu kama utaacha kushauri kila mtu, hata kama hajakuomba ushauri.

Hii ni kwa sababu ni rahisi sana kutoa ushauri kwa wengine, lakini kufanyia kazi ushauri huo huo unaowapa wengine na vigumu.

Changamoto za wengine huwa zinaonekana rahisi na zinazotatulika. Ila changamoto zetu wenyewe huwa zinaonekana ngumu na zisizotatulika.

Tatizo jingine ni hili, kila mtu anajua jinsi ambavyo wengine wanapaswa kuendesha maisha yao, lakini wao wenyewe hawajui jinsi wanavyopaswa kuendesha maisha yao wenyewe.

Utakuta mtu analaumu wengine kwa kosa fulani au udhaifu fulani walionao, lakini na yeye ana madhaifu na makosa mengi, ila tu ya kwake hayajapata nafasi ya kuonekana hadharani.

Yote haya ni kusema, mambo huwa siyo rahisi kama yanavyoonekana kwa nje, na huwa siyo magumu kama tunavyofikiria yanapokuwa yanatukabili.

Hivyo tuchukue hatua sahihi kwa yale yanayotukabili, na tuokoe muda na nguvu zetu kwa kutokusikiliza kila aina ya ushauri au kutoa kila aina ya ushauri.

Mwisho, itakuwa vyema sana ukajua jinsi ya kuyaishi maisha yako, kabla hujataka kuwaambia wengine wanavyopaswa kuyaishi maisha yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha