Vitu viwili ambavyo wengi hawajui jinsi ya kuvitumia kwa usahihi na hivyo vinaishia kuwapoteza badala ya kuwasaidia kufikia mafanikio makubwa.
Kama hujaanza kuchukua hatua, basi kuanza ni bora kuliko kusubiri mkakati bora zaidi. Wengi wamekuwa wakipoteza kwa kusubiri mkakati bora na sahihi kwao. Kila wakati wanapanga na kupangua, wanaona uimara na udhaifu na mwisho wa siku hakuna kinachofanyika. Kama bado hujaanza, kipaumbele cha kwanza kwako ni kuanza. Anza na mkakati wowote, kisha unavyoendelea kufanya utaendelea kuboresha mkakati huo. Kwa sababu, hakuna mkakati wowote utaendelea kama ulivyokuwa umepanga kabla ya kuanza, hata kama ni bora kiasi gani.
Kama tayari umeshaanza kuchukua hatua, basi kuhakikisha uko kwenye uelekeo sahihi ni bora kuliko kuweka juhudi zaidi. Watu wanapenda kuweka juhudi, wanapenda kusema wanafanya kazi masaa mengi, wanalala masaa machache, lakini ukiangalia, hakuna kikubwa wanachozalisha. Hiyo ni kwa sababu juhudi hizo zinapotea kwa mambo yasiyokuwa sahihi. Kabla hujaweka juhudi zaidi, jiulize je kile unachofanya ni sahihi, je kinakufikisha kule unakotaka kufika? Inaumiza sana pale unapoweka juhudi kubwa na kufika mwisho ndiyo unagundua hukuwa njia sahihi.
Kwenye nyumba yako ya mafanikio, juhudi ni sakafu na mkakati ni dari, vitu hivi viwili vinaifanya nyumba yako kuwa nzuri kama vitafanywa kwa usahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,