Kuna wakati unaweza kukasirishwa na maneno au matendo ya mtu fulani, kiasi cha wewe kushindwa kabisa kufanya kazi yako.
Labda ni mtu maarufu au kiongozi mkubwa ambaye ameongea au kufanya kitu kinachokuumiza sana wewe na kikapelekea ukasirike na hata kukata tamaa ya kuendelea kufanya ulichokuwa unafanya.
Unaweza kuchukua muda wako kulalamika, kuonesha kwa nini hayuko sahihi na mengine mengi. Hilo linakukosesha kabisa usingizi, ukiendelea kutafakari alichosema au kufanya.
Lakini kwa upande wa pili, yule ambaye amekufanya wewe uvurugwe, amelala zake usingizi, hana hata wasiwasi. Na kibaya zaidi, hajui kabisa kama kuna mtu anaitwa Amani John ambaye amevurugwa na kukosa usingizi kabisa kutokana na maneno au matendo yake.
Wewe unaumia na kuvurugwa, huku anayekufanya uumie na kuvurugwa akiwa hajui hata kama uko hai.
Hapo hujitendei haki kabisa, ni kuyaharibu na kuyapoteza maisha yako kwa jambo lisilo na maana.
Jukumu lako ni kufanya kazi yako, kuchukua hatua ulizopanga kuchukua. Wengine wanasema au kufanya nini siyo jukumu lako. Iwe wanachosema au kufanya kinakuathiri, wewe weka juhudi zako kwenye kufanya kile ulichopanga kufanya.
Hii haimaanishi ukubaliane na kila anayekuingilia, unapaswa kusimamia kile kilicho sahihi na kama mtu anafanya hivyo kwa kusudi kumchukulia hatua. Lakini usisumbuke na wale ambao hawapo ndani ya uwezo wako kuchukua hatua. Wewe endelea na maisha yako.
Hii inajumuisha zile tabia za kujadili maisha ya watu maarufu au wenye mafanikio makubwa, na kuanza kusema wapi wanapatia na wapi wanakosea, ni upotevu wa muda na maisha yako, maana watu hao hawajui kuhusu uwepo wako, na hayo maoni yako hayawezi kuwafikia.
Kadhalika kuruhusu mambo ya wanasiasa, kuvuruga utulivu wako ni kuchagua kuyaharibu maisha yako. Fanya kile kilicho sahihi, hilo ndiyo muhimu kuliko mengine yote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha ni hekima inayomtoa mtu kifungoni mwake mwenyewe.
LikeLike