Tuna kasumba kama binadamu ya kupenda kubadili vitu pale vinapokuwa vinafanya kazi vizuri na kung’ang’ana navyo pale vinapokuwa havifanyi kazi.

Ni kitu kisichokuwa na manufaa kabisa, lakini huwa tunahangaika sana kukifanya. Na ni kwa kuwa huwa tunapata uchoshi (boredom) pale tunaporudia kufanya kitu kile kile kila siku.

Chukua mfano umeanzisha biashara, wateja wameielewa na wananunua, kila kitu kinaenda vizuri, lakini hutulii, kila wakati unaangalia nini cha kubadili, mwishowe unabadili kile kilichokuwa kinawaleta wateja na wanaacha kuja.

Lakini ukianzisha biashara na ikawa haileti wateja, utaendelea kung’ang’ana nayo hata kama kuna namna unakosea.

Ni jambo la kushangaza sana, lakini ndivyo tulivyo kama binadamu, kitu kikifanya kazi vizuri tunakazana kukibadili, kisipofanya kazi tunang’ang’ana nacho.

Sasa ni wakati wa kwenda kubadili hilo, ili tuache kuwa kikwazo cha mafanikio yetu wenyewe.

Pale unapochukua hatua fulani na matokeo yakawa mazuri, endelea kuchukua hatua hizo bila ya kuacha au kubadili haraka.

Na pale unapochukua hatua na matokeo yakawa siyo mazuri, basi badili hatua unazochukua ili uweze kupata matokeo mazuri.

Kama umewapa watu uchaguzi wa vitu vitatu na wao wakachagua kimoja, weka nguvu zako zote kwenye hicho kimoja ambacho watu wamekichagua, hicho ndiyo wanachotaka na chenye manufaa kwao. Kwa nini ujisumbue na kingine?

Kama umewapa watu uchaguzi wa vitu vitatu na hawajachagua hata kimoja, usiendelee kung’ang’ana na hivyo ukidhani hawajavielewa vizuri, badala yake endelea kuwapa machaguo zaidi mpaka wakutane na wanachohitaji kisha weka nguvu kwenye hicho.

Hii haimaanishi kwamba ukishapata kinachofanya kazi ndiyo uende nacho kwa mazoea bila ya kubadili. Unapaswa kukiboresha kila wakati, kwa namna ambayo inampa mteja thamani zaidi. Lakini siyo kukimbilia kubadili kwa sababu tu umechoka kukifanya kwa jinsi kilivyo.

Rudia kile kinachofanya kazi na endelea kukiboresha zaidi, usikimbilie kukibadili kama ilivyo tabia yetu binadamu.

Badili kile ambacho hakifanyi kazi mpaka upate kinachofanya kazi, using’ang’ane kukifanya kwa namna umekuwa unafanya kama ilivyo tabia yetu binadamu.

Hivi ni vitu vidogo vidogo sana ambavyo unaweza usivielewe lakini vikawa changamoto kubwa kwako kupiga hatua kubwa na kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha