Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye makala ya uchambuzi wa vitabu ambapo unapata kwa ufupi yale muhimu yaliyopo kwenye vitabu mbalimbali. Na pale unapohitaji kupata uchambuzi huo kwa kina, basi unajiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania
Leo tunakwenda kupata uchambuzi wa kitabu kinachoitwa The Black Swan; The Impact of the Highly Improbable. Hiki ni kitabu kilichoandikwa na Nassim Nicholas Taleb ambaye ni mwekezaji, mwanahisabati, mwanafalsafa na mwandishi ambaye amekuwa akiandika vitabu vinavyoangalia uhalisia wa dunia tunayoishi na jinsi wengi wanavyoshindwa kuuona na kuutumia kuepuka kupata hasara.
Kwenye kitabu hiki cha The Black Swan, Taleb anatuonesha athari za matukio ambayo hayategemewi kutokea.
Jina la kitabu hiki linatokana na mazoea yaliyokuwepo duniani kwamba bata maji (swans) wote walikuwa weupe. Ni mpaka karne ya 17 ambapo watu walikutana na bata maji weusi ndiyo waligundua kwamba mazoea siyo uhalisia.
Hivyo Taleb anatumia dhana hii kwamba kuna vitu tumevizoea na kuamini vipo hivyo tu, lakini ukweli ni kwamba kuna vingine, ila hatujawahi kuviona. Sasa kwa kuwa hatutegemei tofauti na tulivyozoea, kinapotokea kile ambacho hatujatarajia kinakuwa na madhara makubwa sana kwetu.
Taleb anatoa mifano ya matukio ya Black Swan ni kama vita vya dunia, anguko la uchumi, kulipuliwa kwa Marekani na magaidi (9/11) na matukio mengine kama hayo ambayo yameleta madhara kwa wengi, lakini hakuna aliyetegemea yatokee.
Kupitia kitabu hiki, Taleb anatushirikisha jinsi ya kuwa na maandalizi bora kwa yale tusiyotegemea, ili yanapotokea madhara yasiwe makubwa kwetu.
Sifa tatu za Black Swan.
Taleb anasema ili tukio liwe Black Swan lazima liwe na sifa hizi tatu;
Moja; liko nje ya mazoea na mategemeo (outlier) kwa sababu halijawahi kutokea tena siku za nyuma.
Mbili; lina madhara makubwa kwa wengi.
Tatu; linaweza kuelezeka baada ya kuwa limetokea na watu kuona kwamba lingeweza kutabirika (lakini hiyo ni baada ya kuwa limetokea).
Zaidi kutoka kwa mwandishi.
Wazo kuu la kitabu hiki ni upofu ambao tunao kwenye mchango wa bahati kwenye mambo mbalimbali yanayotokea. Tuna tabia ya kuona mambo madogo madogo lakini kushindwa kuona mambo makubwa na yenye madhara makubwa. Taleb anasema kufuatilia sana habari kunakufanya ushindwe kuijua dunia vizuri.
Mafanikio yanakwenda kinyume na mazoea na matarajio. Kadiri mtu anavyofanya kile kilichozoeleka na kinachotarajiwa, anakuwa na nafasi ndogo ya kufanikiwa. Lakini anayefanya kile ambacho hakijazoeleka au kutarajiwa, anakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa.
Hakuna mtu anayeweza kutabiri kitu chochote kwa uhakika wa asilimia 100. Wale wanaotabiri na kupatia wanakuwa wamebahatisha tu. Hivyo hatupaswi kuamini na kutegemea utabiri wa mtu yeyote (hata wataalamu) kwa sababu hauna uhakika. Taleb anasema hakuna watu wanaokosea kwenye utabiri kama wataalamu, kwa sababu wanakuwa wanafikiria kile wanachojua wao tu na kutokuona picha kamili.
Tofauti na hadithi nyingi za mafanikio zinavyoeleza, hakuna uvumbuzi wowote, hasa kwenye teknolojia, ambao umetokana na mipango ambayo watu walikuwa wameweka. Uvumbuzi umekuwa unakuja kama ajali, mtu akiwa analenga kufanya kitu kingine na anapata matokeo mengine. Hivyo ili kufanikiwa hatupaswi kutegemea sana kwenye mipango tuliyoweka, bali kuwa huru kuziona fursa mbalimbali zinazotuzunguka.
Kinachotuumiza siyo kile tunachojua, bali kile tusichojua na changamoto kubwa kwetu binadamu ni kutokuwa tayari kujifunza vitu ambavyo vinapingana na kile tunachoamini. Hii inafanya matukio tusiyotegemea kutuumiza sana pale yanapotokea.
Changamoto nyingine kubwa kwetu binadamu ni kwamba huwa hatupendi kufikiri. Kwa sababu kufikiri ni kazi ngumu, inayohitaji muda na inayotumia nguvu kubwa ya miili yetu. Lakini pia watangulizi wetu hawakuwa watu wa kufikiri sana, bali kuendeshwa na hisia. Hivyo tumerithi hilo kwao na linatufanya kuwa dhaifu, hasa kwa matukio ambayo hatujayazoea.
Changamoto kubwa kwenye jamii zetu ni kwamba mashujaa halisia huwa hawasifiwi wala kutukuzwa, bali mashujaa feki. Tukichukulia mfano wa mlipuko unaofanywa na magaidi, kama kuna mtu atajua mipango ya mlipuko huo na akauzuia, hataonekana shujaa na wala hakuna atakayemwandika na kumsifia sana, itaonekana ni kitu cha kawaida. Lakini pale mlipuko unapotokea, ambao umeshaleta madhara, kama kuharibu mali na vifo vya watu, wale wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kusaidia hali hiyo ndiyo wanaitwa mashujaa na kusifiwa sana. Kwa hili jamii haiwatendei haki wale wanaoona madhara ya mbele na kuyazuia, hivyo wengi hawahangaiki kufanya hivyo.
Mabadiliko yote yanayotokea duniani, huwa yanasababishwa na matukio ambayo hayakutegemewa (Black Swans), lakini elimu yetu na mfumo wetu wa maisha, unaangalia yale yanayotegemewa. Ndiyo maana watu hawana maandalizi ya kutosha kwenye matukio yasiyotarajiwa na hivyo kuwa na madhara makubwa.
Kutengeneza maisha unayotaka.
Taleb anatuambia baada ya kuona udhaifu mkubwa uliopo duniani kwenye maarifa unaotokana na historia na utabiri, aliamua kuchagua kutengeneza maisha ambayo anayataka yeye na siyo yale ambayo wengine wanayaishi. Katika kutengeneza maisha anayoyataka, alifanya yafuatayo;
- Kuamua kufanya biashara ya uchuuzi wa hisa, kununua na kuuza hisa kwa kuangalia mwenendo wa soko na uchumi.
- Kuchagua eneo dogo ambalo atalijua kwa undani na kuachana na maeneo mengine, hivyo kupunguza kusumbuka na mambo mengi.
- Kuokoa muda wake kwa kutokuhudhuria kabisa vikao na mikutano yoyote ya kibiashara.
- Kuepuka kujiunga na taasisi au kikundi cha aina yoyote ile, hivyo kuwa huru kufanya mambo yake mwenyewe.
- Kuepuka kujihusisha na watu ambao hawasomi vitabu.
- Kuchukua mapumziko ya mwaka mmoja (sabbatical) kila baada ya miaka mitatu ili kufukia mashimo yaliyopo kwenye falsafa yake ya kazi na maisha.
- Kuchagua kuwa huru kufanya kile anachotaka na pale anapotaka kukifanyia badala ya kulazimika kuwa ofisini muda wote.
- Kulala kwa muda anaotaka yeye, ambao unamtosha.
- Kuwa huru kusoma atakavyo.
- Kutokuwajibika kujieleza au kujitetea kwa yeyote.
Kwa uhuru huu, Taleb ameweza kuandika vitabu ambavyo vimeleta mapinduzi makubwa kwa namna watu wanavyofikiri na kufanya maamuzi yao. Pia ameweza kuwa anaona majanga kabla hayajatokea na kutokudhurika nayo.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, tujifunze kuhusu athari za matukio yasiyotarajiwa na jinsi ya kuwa na maandalizi ya kutosha pale matukio hayo yanapotokea. Anachotuambia Taleb ni kwamba hatuwezi kuzuia yasiyotarajiwa yasitokee, hatujui ni wakati gani yatatokea, lakini kuwa tayari wakati wote, tunaweza kunufaika na matukio hayo badala ya kudhurika.
Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki, ambao una sehemu nne, ingia kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA na upakue chambuzi hizo pamoja na kitabu chenyewe. Kujiunga na channel hiyo hakikisha una programu ya Telegram kwenye simu yako au kompyuta yako kisha fungua www.t.me/somavitabutanzania na bonyeza JOIN CHANNEL hapo utakuwa umejiunga na utaweza kupata chambuzi nyingi za vitabu mbalimbali.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kama ungependa kuwa karibu zaidi na kocha, kujifunza kwa kina na kupata mwongozo na ushauri wake, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni programu ya ukocha ambayo inakupa mafunzo na mwongozo wa kufanikiwa zaidi kwenye maisha. Kujiunga tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 na utapewa maelekezo ya kujiunga.