Kila mtu anajua vitu gani sahihi kwa wengine kufanya, ila hakuna anayejua anachopaswa kufanya yeye. Hivyo ni rahisi kushauri na hata kukosoa wengine, kuliko kujijengea nidhamu ya kufanya kile unachopaswa kufanya.
Leo ni muhimu kujikumbusha yapi majukumu yetu na yapi siyo majukumu yetu.
Jukumu lako ni kufanya kile kilicho sahihi, kitakachokuwezesha kufika kule unakotaka kufika, na chenye manufaa kwako na kwa wengine pia. Hilo tu ndiyo muhimu zaidi kwako, mengine yote ni kujisumbua na kupoteza muda wako.
Wengine wanafanya nini na iwe wanafanya kwa usahihi au la hilo siyo jukumu lako. Ukianza kufuatilia kila mtu anafanya nini kama vile wewe ndiyo umepewa upolisi wa dunia nzima, utajichelewesha sana kupiga hatua.
Kwenye kila hali unayojikuta, jiulize ni kipi sahihi kufanya kwenye hali hiyo. Hata kama umejikuta njia panda, usikubali kukwama, jiulize kipi sahihi kufanya, kipi kitakuwa na manufaa kwako na kwa wengine pia, kipi unaweza kukiboresha zaidi ya kilivyo sasa.
Kwa kufanya hivi haimaanishi kwamba utapatia mara zote, utakosea, lakini utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujifunza na kuwa bora zaidi.
Popote unapokuwa, jaribu kufanya kitu kuwa bora kuliko kilivyokuwa awali, hii itakupa fursa nyingi zaidi za kupata kile unachotaka kuliko kuwa mtu wa kulalamika na kufuatilia maisha ya wengine.
Jikumbushe hili kila siku na kila wakati unapoanza kufanya chochote, jukumu lako ni kufanya kilicho sahihi, kufanya kitu kiwe bora kuliko kilivyokuwa awali, kutoa thamani zaidi. Mengine waachie wengine, maana nguvu na muda ulionao hautoshi kwako kuhangaika na mambo mengi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,