“Ever since the world began, men have been subject to various tricks of Fortune, and it will ever be thus until the end.” – Giovanni Boccaccio

Tangu kuanza kwa ulimwengu, binadamu wamekuwa wanapitia changamoto na majanga mbalimbali yanayotokana na asili.
Na hivyo ndivyo itakavyokuwa kila siku ya maisha ya mwanadamu hapa duniani.
Katika kipindi chote ambacho dunia itakuwepo, changamoto na majanga yatakuwa ni sehemu ya maisha.
Tukivuka changamoto moja tunakutana na nyingine.
Tukimaliza janga moja, jingine kubwa zaidi linakuja.

Hivyo usiombe au kutamani changamoto na majanga visitokee,
Badala yake kazana kuwa bora zaidi, kiasi kwamba unaweza kukabiliana na changamoto au janga lolote litakalotokea kwenye maisha yako.
Hii ndiyo njia bora kwaku kupiga hatua licha ya magumu mbalimbali unayoweza kukutana nayo.

Maisha haya tumepewa kama zawadi,
Na zawadi hiyo ina vigezo na masharti,
Na moja ya masharti ni kwamba katika nyakati usizojua wala kutegemea, utakutana na changamoto au janga kubwa,
Lakini itakuwa ndani ya uwezo wako kuvuka changamoto na majanga hayo.
Kama umeipokea zawadi hii ya maisha, basi jua vigezo na masharti vitazingatiwa.
Kuwa tayari kukabiliana na changamoto au majanga muda wowote kwenye maisha yako.

Tatizo letu wanadamu ni tusipopata changamoto au majanga kwa muda mrefu huwa tunajisahau.
Na hata kujidanganya kwamba sisi ni wajanja, tumeweza kushinda changamoto na majanga.
Na hapo ndipo asili hutupiga na changamoto au janga kubwa ili tuache kujidanganya na tuelewe kweli uwezo wetu uko wapi na udhaifu wetu uko wapi.
Unapopitia changamoto au majanga,
Fanya kile sahihi na unachopaswa kufanya,
Halafu mengine iachie asili na muda.
Kama unachofanya hakitaitatua changamoto au kuondoa janga,
Basi muda utafanya hivyo kwa ajili yako.

Magumu, changamoto na majanga ni sehemu ya maisha.
Usitamani maisha yasiyo na vitu hivyo, bali tengeneza maisha yanayoweza kukabiliana navyo bila ya kukata tamaa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania