“Quiet minds cannot be perplexed or frightened but go on in fortune or misfortune at their own private pace, like a clock during a thunderstorm.” — Robert Louis Stevenson

Kama kuna dhoruba kali ambayo inaendelea, unafikiri mishale ya saa inaendaje?
Je itakwenda haraka au polepole?
Jibu unalijua, mishale ya saa itaendelea na mwendo wake bila ya kujali ukali wa dhoruba inayoendelea.
Saa haijiambii kwamba inabidi isubiri kwanza dhoruba itulie ndiyo iendelee na mwendo wake.

Hivyo pia ndivyo watu wenye hekima huendesha maisha yao.
Huwa na akili tulivu ambazo hazibadilishwi na chochote kinachoendelea.
Huendelea kuwa na utulivu na kufanya yale waliyopanga kufanya, bila ya kujali ni kitu gani kinachoendelea.
Hali iwe nzuri au mbaya, wao huendelea kufanya yao.

Usitumie changamoto yoyote unayopitia kama sababu ya kutokufanya kile sahihi kwako kufanya.
Kwa kuwa maisha yako hayatakoma kuwa na changamoto,
Kuyasubirisha mpaka changamoto ziishe ni kuchagua kutokuishi, wakati maisha hayakusubiri wewe uwe tayari.

Kuwa na akili tulivu, isiyoshangazwa wala kutishwa na chochote kinachoendelea.
Wewe endelea kufanya yale uliyopanga, ili kufika kule unakotaka kufika.
Kama kuna ulazima, badili namna unavyofanya, lakini siyo uache kufanya kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania