Ukimwajiri mtu pasipo kumpa mwongozo wa kazi atafanya vile anavyojua yeye ndivyo ilivyo kwa binadamu atafanya vile anavyojua yeye kama wewe unayefanyiwa kazi usipotoa mwongozo wa kazi hiyo.

Hata katika malezi ya watoto wanatakiwa kupewa mwongozo mapema wewe kama mzazi mtoto wako anapaswa kujua kabisa ni vitu gani unapenda na vitu hupendi afanye. Akishajua nini unapenda na nini hupendi atajitahidi kutii lakini asipojua atakua anafanya vile anavyojua yeye mwenyewe.

Leo ninakwenda kukushirikisha mbinu ya kisomo itakayokusaidia katika malezi ya mtoto wako. Mbinu hii ya kisomi ni mbinu ya kimaandishi ambayo unamwandikia mtoto wako mkataba. Yaani wewe kama mzazi mnawekeana mkataba na mtoto katika kile mlichokubaliana kifanyike.

Create a Homework Contract Between Parents and Tweens

Kwa mfano, unaweza kukaa na mtoto mmoja mmoja kama unao zaidi ya mmoja ukaongea naye na kujua kile kinachoendelea ndani yake. Ukampatia mwongozo ambao anapaswa kuishi na kuusimamia au kuna majukumu ambayo anatakiwa afanye ili kuepuka kusahau unamwandikia mkataba yaani mnakaa chini unamwandikia kile ambacho anapaswa kukifanya na chini wewe unaweka saini yako na yak wake pia kuonesha kuwa amesoma na ameelewa kile anachotakiwa kufanya yeye kama mtoto.

Mkataba huo unapaswa kuwa na tarehe na miiko ambapo kama akienda kinyume na kile mlichokubaliana atakutana na athari gani. kwenye mkataba huo wa makubaliano usifiche kitu kila kitu weka wazi.

Kila mmoja awe na nakala yake, ikiwa yeye amesaini na wewe umesaini. Ikiwezekana aweke kwenye faili lake au abandike ukutani au mlango ili kila anapouona mkataba wake unamkumbusha majukumu yake.

Usipompatia mtoto mwongozo hata akikosea hawezi kujua kama amekosea lakini ukimuonesha nini anatakiwa kufanya anakuwa na nidhamu. Kwa mfano, kama unata mtoto ambaye unaona tabia au mwenendo wa hauko sawa, kaa naye mweleze kuwa mwenendo wake hauko sawa, kubalianeni hatua mtakazo chukua kukabiliana na hilo na baada ya kukubaliana nendeni kisomi, andikishaneni mkataba wenu wa kufikia maamuzi hayo.

Maeneo mengi ya kazi, watu baada ya kukubaliana jambo kama ni kupeana kazi, mnaingia mkataba na mkataba unamuonesha kila mtu anavyopaswa kuwajibika na nini kitafanyika baada ya kwenda kinyume na mkataba mliyowekeana?

Mwandike mtoto majukumu yake anayotakiwa kuyajua na kisha andikianeni mkataba huo wa makubaliano na kila mmoja aweke saini katika makubaliano yetu mliyofikia kwa ajili ya utekelezaji. Mnapoandikishiana mkataba anaona kweli wewe mzazi uko makini na hilo jambo siyo la utani mpaka mnafikia hatua ya kuandikishana.

Mtaheshimiana, unamjengea uwezo mkubwa wa kujiongoza kupitia kile mlichokubaliana, baada ya kumpatia majukumu yake na kuyaainisha kwenye mkataba usiendelee kumkumbusha tena kile anachotakiwa kufanya kwa mdomo wewe fuatilia na mwache ajiongoze mwenyewe uone kama kweli anaweza kujiongoza mwenyewe kadiri yale mliyokubaliana kwenye mkataba.

Hatua ya kuchukua leo; nenda ukae na mtoto wako, ukubaliane naye kile unachotaka awe anafanya iwe ni mambo ya shule au nyumbani. Unaweza ukamwambia, nataka shuleni upate wastani wa A, badala ya kukubaliana kwa mdomo nendeni kimaandishi kabisa ajue kile unachotaka na kisha akiri kimaandishi na kusaini kupitia mkataba wenu mliyojiwekea.

Kwahiyo, watu wanapenda kujituma pale unapokuwa unawapa lengo la kufikia, hata mtoto wako ukimpatia malengo ya kufikia, mkawekeana mkataba, akasaini atajituma kufikia kile mlichokubaliana ili kuepuka kuoenekana mzembe na mvivu. Usipompa mtoto lengo la kufikia unakua unamwacha njia panda, malengo yanampatia mtoto hamasa ya kujituma zaidi. Tumia mbinu hii kwa mtoto au watoto wako na utakua mnafikia mafanikio makubwa.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana