Changamoto kubwa tunayokutana nayo kwenye maisha yetu ni kushindwa kuweka vizuri vipaumbele vyetu. Kila mmoja wetu ana udhaifu kwenye hili, unajikuta umepanga au kukubali kufanya vitu vingi kuliko uwezo wako au muda ulionao.
Tumeshajifunza sana dawa ya hili, ambapo ni kutumia neno HAPANA mara nyingi uwezavyo. Yaani pale unapokutana na kitu ambacho unashawishika kukubaliana nacho, lakini hakipo kwenye vipaumbele vyako unasema hapana.
Sasa hii ni rahisi kusema kwenye wakati uliopo (sasa) lakini ni ngumu sana kwenye wakati ujao. Mtu anaweza kuja kwako na kukupa pendekezo fulani lakini kwa siku zijazo, kwa kuwa unaona ni siku zijazo, unasema ndiyo.
Baadaye unakuja kugundua umesema ndiyo kwenye vitu vingi kiasi kwamba hupati muda wa kufanya yale muhimu kwako.
Njia bora ya kuepuka hili ni kutumia muda ulionao sasa. Pale mtu anapokuja kwako na ombi au pendekezo linalokuhitaji wewe kwa siku zijazo, kabla hujasema ndiyo jiulize kwanza swali hili; kama ungepaswa kufanya sasa, je ungekubali.
Kwa swali hili, unapima kweli kipaumbele cha kitu hicho kwenye wakati uliopo, leo hii tayari umeshajiwekea vipaumbele vyako, hivyo huwezi kukubali kile ambacho hakiendani na vipaumbele hivyo. Kwa chochote unachoshirikishwa kwa siku zijazo, jiulize kama ungetakiwa kufanya leo, je ungeacha yale uliyopanga na kukifanya?
Kama jibu ni hapana, kwamba huwezi kufanya leo, basi jua pia hutaweza kufanya siku zijazo, hivyo sema hapana. Haijalishi utajiambia kwamba siku zijazo utakuwa na nafasi ambayo leo huna, huo siyo ukweli, kama huna nafasi ya kufanya kitu leo, hutakuwa nayo kesho wala siku zijazo.
Unafikiri kwa nini ukijiambia utafanya kitu kesho huwa ni vigumu kukifanya? Kwa sababu kama umeweza kukiahirisha, basi siyo muhimu, kama kimekosa muda kwenye siku yako ya leo, basi hicho siyo muhimu kama vingine vilivyopata muda.
Hivyo acha kujidanganya na kujiongezea changamoto kwenye siku zijazo, kama kitu haupo tayari kukifanya leo, usikubali kwamba utaweza kukifanya siku zijazo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,