Mpendwa rafiki yangu,

Tuna ile nadharia fulani inayosema, fanya kama ninavyosema na siyo ninavyotenda. Kupitia nadharia hii wazazi wengi wamepoteza uaminifu kwa watoto wao.

Watoto wetu huwa wanajifunza kila kitu kutoka kwetu pale wanapokuwa wadogo ila sisi tunakua kama vile hatujali hilo. Tumekuwa na watoto ambao tabia zao haziendani kabisa na wazazi na mpaka muda mwingine mzazi anajiuliza hizi tabia mtoto amezipata wapi, watu waliomzunguka mtoto wanachangia kujenga au kubomoa tabia ya mtoto wako.

Mwalimu wa kwanza wa anayemfundisha mtoto wako uongo ni wewe mwenyewe. Kivipi namfundisha mtoto wangu kusema uongo?

Jibu, moja, kwa kushindwa kutekeleza kile unachoahidi kwa mtoto wako tu.

Pili, Unamfundisha kwa maneno tu lakini matendo yako yanakwenda kinyume na kile unachosema.

Kwa njia hizi mbili tunakua tuna haribu kabisa watoto wetu, kwa mfano, ni wazazi wengi sana wanawaahidi watoto wao vitu ambavyo hawawezi kuvitekeleza na kama unavyojua watoto ni watu wenye imani kali chochote wanachoambiwa na mzazi wanaamini wanakwenda kupewa hivyo usipofanya unajenga uongo ndani yao na ndiyo maana hata baadaye mtoto anakuja kuwa mwongo wewe mwenyewe unashangaa kumbe mwalimu ni wewe mwenyewe.

Kuwa makini na kile unachoahidi katika malezi ya mtoto wako kwani kinakwenda kumjengea uaminifu au kubomoa.

Pili tenda kama ulivyosema, kwa mfano hakuna kuangalia TV watoto huu ni muda wa kusoma, unawaambia watoto wasome wewe unaangalia TV, badala hata kusoma nao na wewe ushike kitabu usome bali unakuwa bize na TV ambapo wenzako wanaingiza siku na wewe unatakiwa kuitumia kwa manufaa ya mtoto wako.

Kipindi hiki cha Corona, wako wazazi ambao hawana hata muda na watoto wao licha ya kuwa nyumbani. Watoto hawasaidiwi kimasomo lakini utamkuta mzazi huyo huyo anajisifu yaani unajikuta unaangalia muvi mpaka unachoka. Muda wa TV anao lakini wa kujenga watoto hana baadaye watoto wakiharibika anakuja kutumia gharama kubwa tena na kulipa riba.

Ewe mzazi amka, acha mambo ambayo hayamsaidii mtoto wako mlee mtoto vizuri katika njia ambayo hataicha hata akiwa mzee.

Muda mwingine simu inaita, tunawaambia watoto wapokee simu na wajibu kuwa sema baba au mama hayupo ametoka ameacha simu wakati wewe uko hapo hapo je kwa mtindo huo huoni unakuwa unamfundisha mtoto uongo?

Mzazi ambaye maisha yake yanakuwa ni ya maigizo hata mtoto naye anakuwa hivyo hivyo, nioneshe mzazi mwenye show off (kujionesha) nami nitakuonesha mtoto mwenye show off. Watoto wanakua vile ambavyo sisi tunakua.

Unamwabia mtoto usivute sigara halatu wewe mwenyewe unakua wa kwanza kumtuma akakununulie sigara na kuvuta mbele yake.

Unamwambia mtoto asiwe mlevi wakati wewe ni mlevi.

Unamwambia mtoto wako awe mwaminifu katika maisha ya ndoa wakati wewe siyo mwaminifu katika maisha ya ndoa.

Unawaambia watoto waamke mapema wakati wewe ni mvivu wa kuamka.

Hatua ya kuchukua leo; mzazi kuwa kioo cha mtoto wako.
Fanya kile ambacho ni sahihi kufanya katika malezi ya watoto.
Fanyia kazi kile ulichojifunza hapa na ishi kwa uhalisia wala usiigize maisha maana hata watoto wako wanajua ukweli wa mambo ulivyo.

Hivyo basi, wewe kama mzazi au mlezi unapaswa kuwa makini kuanzia kile unachoongea au kutenda kwa watoto wako kwani wewe ndiyo mwalimu mzuri wa kujenga au kubomoa kwa mtoto wako au hata wengine. Kuwa mfano bora wa kuigwa, jenga familia yako iwe bora na tutakua na jamii bora.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com//kessydeoblog@gmail.com

Asante sana