Watu wengi wanapenda kuajiriwa kuliko kujiajiri wenyewe au kufanya biashara. Hii ni kwa sababu ajira huwa zinaonekana zina usalama mkubwa kuliko kujiajiri au biashara.

Kipindi cha nyuma hilo lilionekana lina ukweli ndani yake, lakini sasa linaonekana wazi kwamba siyo sahihi, usalama wa ajira unaweza kuonekana kwa nje, lakini ndani siyo kweli.

Sasa tukirudi kwenye kujiajiri na biashara, wengi huwa wanaona hakuna usalama, ni kama pata potea. Unaweza kuwa na biashara leo na kesho isiwepo. Lakini hilo sahihi, upo usalama mkubwa kwenye kujiajiri au biashara kama ukiweza kuelewa na kuutumia, utakusaidia sana.

Usalama wa kazi kwenye biashara na kujiajiri ni mteja mwenye furaha. Ukiweza kuwa na wateja wenye furaha, una uhakika wa kuwa na biashara hiyo kwa muda mrefu. Wateja wenye furaha ni wale ambao wameridhika na kile unachowauzia, wanapata thamani na wapo tayari kulipia thamani hiyo.

Unapowahudumia wateja wako vizuri, unajilinda wewe na biashara yako, kwa sababu wanapopata huduma ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine, wataendelea kuja kwako.

Lakini kama utachagua kufanya biashara yako kawaida, kama utaona wateja ni wasumbufu na hutaweka juhudi kuwahudumia vizuri, watatafuta sehemu nyingine ya kwenda kununua na hapo utakosa usalama kwenye biashara unayoifanya.

Kumbuka hili kila siku, usalama wako kwenye biashara na kujiajiri ni mteja mwenye furaha, hivyo jukumu lako ni kutengeneza wateja wengi wenye furaha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha