“The greatest joy, according to the works of Francis Assisi, is that you can endure everything, you can even suffer slander and physical pain, and at the end you are able to feel no animosity toward these sufferings, but you feel joy, because you have faith; such joy cannot be destroyed, either by evil people or by your own suffering.” Leo Tolstoy

Furaha iliyo kuu ni kwamba unaweza kuvumilia kitu chochote.
Unaweza kuumizwa, kuteswa, kudhalilishwa na hata kukwamishwa,
Lakini mwisho wa siku huwezi kuwa na chuki kwa mateso hayo uliyopitia.
Badala yake unapata furaha iliyo kuu, kwa sababu una imani.
Furaha hiyo haiwezi kuharibiwa na chochote, siyo watu waovu wala mateso unayopitia.

Hili ni jambo muhimu sana kulijua na kuliishi kila siku,
Kwa sababu magumu na changamoto mbalimbali tunazopitia kwenye maisha hazitakuja kuisha kabisa.
Tukitatua moja na kuishinda, nyingine kubwa zaidi inakuja.
Ule wakati ambapo tunaona kila kitu kinakwenda vizuri ndiyo hapo hapo kinatokea kitu cha kutuonesha ni kwa namna gani mambo hayako vizuri kama tunavyodhani.

Kikubwa kabisa ni kuhakikisha hupotezi imani yako,
Imani kwamba unauwezo wa kuvuka chochote kinachokuja mbele yako,
Imani kwamba kesho itakuwa bora kuliko leo,
Imani kwamba kila gumu unalokutana nalo lina namna ya kulivuka,
Imani kwamba mlango mmoja ukijifunga, kuna mwingine unafunguka.
Imani kwamba kisichokuua kinakufanya kuwa imara zaidi.

Ukishakuwa na imani isiyotetereka,
Na ukawa tayari kuchukua hatua kwa lolote unalokutana nalo,
Wakati wote utakuwa na furaha iliyo kuu, bila ya kujali unapitia nini.
Wakati wengine wanalalamika na kukata tamaa, wewe unafurahia.
Maana unajua chochote unachopitia, utaweza kukivuka na maisha yakaendelea.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania