Kwa kile tunachopitia sasa, jukumu kubwa ulilonalo ni kuepuka kabisa hali yoyote ambayo ni hasi.
Kama kuna watu ukiongea au kuwasiliana nao wanaongea mambo hasi na kulalamika jinsi mambo yalivyo magumu, acha mara moja kuongea au kuwasiliana nao.
Kama kuna vyombo vya habari au vipindi ambavyo ukifuatilia unakutana na taarifa hasi na za kukatisha tamaa, achana na vyombo hivyo.
Kama kuna mitandao ukiitembelea unakutana na habari hasi na za kukatisha tamaa, acha kuitembelea.
Kama kuna watu mitandaoni ambao ukiwafuatilia unapata hali ya kukata tamaa, acha kuwafuatilia watu hao mara moja.
Kuchagua kuepuka hali hizi hasi siyo kwamba unajidanganya tatizo halipo.
Tayari unajua tatizo lipo, sasa kuendelea kukumbushwa kuhusu tatizo hilo kila wakati itakusaidia nini?
Tayari unajua watu wanakufa kwa ugonjwa huu, sasa kufuatilia ujue ni wangapi wamekufa leo inakuongezea wewe nini?
Tatizo lipo, chukua tahadhari unazopaswa kuchukua, kisha achana na habari, watu au hali zozote hasi, zinazokuhubiria tatizo kila siku, zinazokupa hofu zaidi.
Wewe ishi kila siku kwa ukamilifu wake,
Umeiona leo, ishi leo, shukuru kwa siku hii ya leo, fanya yale uliyopanga kufanya leo, toa thamani zaidi leo, wajali wale muhimu kwako leo. Na hutabaki na muda wa kuhangaika na mambo hasi.
Zoezi hili ni gumu kufanya kwa sababu sisi binadamu huwa hatupendi kuachwa nyuma, hatupendi kupitwa,
Tunataka kujua kila kinachoendelea,
Tunataka kujua nani anaumwa na nani amekufa.
Hivyo lazima ujilazimishe kuachana na hayo,
Peleka muda wako, nguvu zako na umakini wako kwenye mambo yenye tija kwako,
Kuishi maisha yako na kufanya kazi yako.
Ishi kila siku yako kwa ukamilifu wake,
Na kama utaipata nafasi ya kuishi siku nyingine, shukuru na iishi kwa ukamilifu wake pia.
Epuka kabisa kila hali hasi na tutaweza kuvuka pamoja katika kipindi hiki.
Kocha.