Mafanikio yanahitaji ukomavu wa hali ya juu sana. Ndiyo maana kuna baadhi ya watu huwa tunawaona wakiwa wameyakaribia kabisa mafanikio yao, lakini wanapoteza kila kitu.
Labda ni msanii amekutana na umaarufu wa ghafla, au mfanyabiashara amekutana na fursa ya kipekee inayompa faida sana, au mfanyakazi amepata nafasi ya kuwa kiongozi. Wengi wanaopata nafasi za aina hii, ambazo ni milango mizuri kwao kufanikiwa, wamekuwa wanazipoteza.
Kupotea kwa nafasi hizi huwa wanatoa sababu mbalimbali lakini huwa hawagusi sababu halisi, ambayo ni uchanga.
Watu wanazipoteza nafasi nzuri wanazokuwa wamezipata kwa sababu ya uchanga, kwa sababu hawajawa na ukomavu wa kuweza kuhimili nafasi hizo.
Hapa tunakwenda kujifunza dalili za uchanga, ili ujihakikishie unaondokana nazo na zisiwe kikwazo kwako kufanikiwa zaidi.
Kutaka kushinda kwenye kila jambo, hata mambo madogo na yasiyo na manufaa. Hii ni dalili kubwa ya uchanga ambayo imewaangusha wengi, kutokana na nafasi ambayo mtu anakuwa ameipata, anaona anapaswa kushinda kila jambo, na hapo anaangushwa na mambo madogo yasiyo na manufaa yote kwake.
Kushindwa kuomba samahani pale ambapo mtu anakuwa amekosea au kukwaza wengine ni dalili ya uchanga. Kwa sababu mtu amepata nafasi fulani anaona yuko juu ya wengine wote, hivyo hata anapofanya makosa au kukwaza wengine, anaona hawezi kuwaomba samahani. Kwa njia hii anaharibu mahusiano mengi.
Kuangalia matokeo ya muda mfupi badala ya muda mrefu. Watu wengi wanapopata nafasi fulani, wanachoangalia ni kubaki kwenye nafasi hiyo na kutokuanguka, hawaangalii kwenda nafasi ya juu zaidi. Hivyo wanachofanya ni yale ambayo yanaleta matokeo ya muda mfupi na yanayoonekana haraka kuliko yale yanayoleta matokeo ya muda mrefu. Kinachotokea ni kuanguka kwa kuwa matokeo ya muda mfupi huwa hayadumu.
Dalili nyingine za uchanga ni kufanya mambo ili kuonekana na kupata umaarufu, kuweka nguvu kubwa kwenye kujionesha kuliko kwenye kufanya kazi na kujiona wewe ni bora kuliko wengine.
Zipo pia dalili kama kuona umeshajua kila kitu hivyo huna kipya cha kujifunza, na hii ndiyo inawaangusha walio wengi, hasa wakishapata mafanikio kidogo. Wakati wanaanzia chini wengi huwa tayari kujifunza na kujituma, ila wakishapiga hatua fulani wanajiona wameshajua kila kitu na hakuna cha kujifunza, na hapo ndipo anguko lao linapoanzia.
Ondokana na kila tabia ya uchanga uliyonayo, jijengee ukomavu ambao utakuwezesha kupata mafanikio makubwa na kudumu na mafanikio hayo.
Dalili kuu ya ukomavu ni unyenyekevu, ukijijengea unyenyekevu, tabia nyingi za uchanga zitakimbia zenyewe. Hutahangaika kushinda kila aina ya jambo, utakuwa tayari kuomba samahani, utakuwa tayari kujifunza na utawaheshimu wengine pia.
Mafanikio bila ya unyenyekevu ni kaburi ambalo linamzika kila mtu, liepuke sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,