Kwenye changamoto tunayopitia na hata nyingine nyingi,
Ni rahisi sana kila wakati kuwa imetingwa na mambo mbalimbali.
Yaweza kuwa kazi zako mwenyewe,
Inaweza kuwa taarifa mbalimbali za yale yanayoendelea,
Au kwa kuwa na muda mwingi, unajikuta unamaliza wote kwa kuzurura mitandaoni au kuangalia tamthilia na maigizo mbalimbali.
Kitu ambacho tunakikwepa sana kwenye nyakati kama hizi ni upweke na utulivu.
Tunatumia kila njia kuhakikisha tunakwepa hali hizo.

Ukweli ni kwamba, hakuna wakati ambapo tunahitaji kupata muda wa upweke na utulivu kama wakati wa changamoto.
Huu ni muda ambao unakuwa peke yako, na siyo kwa ajili ya kufikiria, bali kwa ajili ya kujisikiliza.
Ni muda ambao unakaa na wewe mwenyewe, na kusikiliza nafsi yako.
Unapokuwa umetingwa na mambo mbalimbali,
Nafsi yako huwa inajaribu kukusemesha, kukuonesha fursa bora kwako,
Lakini huisikii kwa kuwa umevutugwa na mengi.
Sasa unapopata muda wa kuwa mpweke na tulivu, unaisikia vizuri nafsi yako, na kuielewa pia.

Katika kipindi tunachopitia sasa, tenga muda ambao utakuwa peke yako, kwenye mazingira ambayo ni tulivu.
Pasiwe na mtu yeyote wala chombo chochote cha mawasiliano.
Ukipenda unaweza kuwa na kalamu na karatasi.
Kisha isikilize nafsi yako,
Sikia kile kilicho ndani yako,
Acha mawazo yako yazurure yawezavyo, lakini usiyaruhusu kwenda kwenye mambo hasi au kuhofia.
Nafsi yako ina mengi sana, ukiisikiliza utaona hata majibu ya changamoto mbalimbali unazopitia.
Unapomaliza zoezi hili, unaweza kuandika yale uliyojifunza au kuyaona, kisha kuendelea na mambo yako mengine.

Tenga muda wa kuwa mpweke na tulivu, isikilize nafsi yako na utaziona fursa na njia bora kwako kuvuka kipindi hiki ukiwa imara zaidi.
Kocha.