Hili ni swali ambalo hupaswi kumuuliza yeyote, wala halipaswi kukusumbua.

Kwa asili yetu binadamu, huwa tunakimbilia kuuliza swali hili pale wengine wanapokuwa hawatupi uzito ambao tunaona tunastahili kupewa. Pale wengine wanapokuwa hawatuheshimu kama tunavyotaka watuheshimu.

Kitu ambacho tunashindwa kuona ni kwamba, kuuliza swali hilo hakusaidii chochote. Kama watu hawakujui wewe ni nani na wanahitaji ujieleze kila mara, ina maana kwamba hawajaona au hawajui kile unachofanya. Hivyo kosa siyo lao, bali ni lako.

Kama watu hawajui wewe ni nani ni kwa sababu hawajui kile unachofanya au unachofanya hakigusi maisha yao. Kama kile unachofanya kinagusa maisha ya mtu, lazima atajua wewe ni nani na lazima atakupa uzito unaostahili.

Hivyo wajibu wako siyo kujieleza kwa kila mtu wewe ni nani, wala siyo kutaka kila mtu akuheshimu au kukupa uzito unaoona unastahili kupewa.

Bali wajibu wako ni kuifanya kazi yako kwa viwango vya juu, kukazana kutoa thamani zaidi kupitia kile unachofanya. Na kwa njia hii, wale walio sahihi kwako watakujua wewe ni nani.

Kama watu wanakuchukulia poa, kama hawakuheshimu kama unavyotaka, peleka hasira zako kwenye kazi, badala ya kupeleka nguvu na muda kujieleza zaidi kwa watu hao, peleka kwenye kufanya kazi yako na kutoa thamani kubwa zaidi.

Matokeo yanasema kwa sauti na yanaeleweka kuliko maneno matupu. Wekeza kwenye kutoa matokeo sahihi kwako. Pia kumbuka siyo lazima kila mtu akujue, bali unapaswa kujulikana na watu sahihi kwako na maisha yako kwenda vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha