“The greatest changes in the world are made slowly and gradually, not with eruptions and revolutions. The same things happen in one’s spiritual life.” – Leo Tolstoy

Mabadiliko makubwa na bora kwenye maisha yako, huwa yanatokea taratibu na kidogo kidogo, siyo haraka na kwa pamoja.
Ukuaji wa kiroho pia huwa unatokea taratibu na kidogo kidogo, siyo kwa ghafla.
Kadhalika kwenye mafanikio makubwa na utajiri, vinahitaji muda kujijenga vizuri.
Dhana ya mafanikio ya haraka ipo kwa matapeli tu kama njia ya kuwalaghai watu wawape wanachotaka.
Lakini kwenye uhalisia, hakuna mafanikio ya haraka.
Hata pale unapoona mtu kapiga hatua kubwa sana ndani ya mwaka mmoja, jua kuna miaka zaidi ya 10 ambapo alikuwa anafanya maandalizi na hakuona chochote kikubwa.

Hii ni kanuni ya asili, mambo makubwa na makuu yanachukua muda.
Angalia kwenye mimea, panda mbegu ya mchicha na ndani ya siku chache itakuwa imeota, ndani ya wiki chache mchicha unakuwa umekomaa kwa ajili ya kula na baada ya muda mfupi maisha yake yanafika ukingoni.
Lakini mbuyu unachukua muda sana kwa mbegu tu kuchomoza, halafu miaka mingine kwenye kukua kabla haujakomaa, lakini baada ya kukomaa, unaishi miaka mingi ukizalisha.
Angalia kwa upande wa wanyama,
Mimba ya panya ni wiki chache tu amezaliwa, na maisha yake ni hivyo hivyo, hawaishi miaka mingi.
Mimba ya binadamu ni miezi mingi, na maisha nayo ni miaka mingi.

Msingi wa ghorofa unachukua muda mrefu na gharama kubwa kuliko msingi wa nyumba ya kawaida.
Chakula kinachoivishwa haraka huwa siyo kitamu.

Kila kilicho kikuu kinahitaji muda ili kujijenga na kutunza nguvu za kuweza kutumika kwa muda mrefu.
Ukikilazimisha unaondoa ukuu wake na hakikupi manufaa.
Jua mafanikio unayotaka kupata na jua ni muda na gharama kiasi gani unapaswa kuweka kabla hujapata unachotaka.
Kisha lipa muda na gharama hizo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania