Who is a wise man?—He who studies all the time.
Who is strong?—He who can limit himself.
Who is rich?—He who is happy with what he has.
—The TALMUD

Mtu mwenye HEKIMA ni yule ambaye anajifunza kila wakati.
Mtu mwenye NGUVU ni yule ambaye anaweza kujidhibiti mwenyewe.
Mtu TAJIRI ni yule ambaye anafurahia kile alichonacho.
Hii ni kanuni rahisi ambayo ukiishi kila siku utakuwa na maisha bora sana.

HEKIMA.
Mwanafalsafa Socrates aliwahi kuulizwa kwa nini yeye ni mtu mwenye hekima kuliko wengine wote.
Akajibu kuna kitu kimoja anakijua, ambacho ni hakuna anachojua, hivyo kila wakati anajifunza.
Wengi tukishajifunza kidogo tunaona tayari tunajua kila kitu, na hapo ndipo tunapokoma kuwa na hekima na kuanza kuporomoka kwenye maisha.
Jifunze kila wakati, kupitia vitabu, mazingira, watu wengine na hali mbalimbali unazopitia.
Kamwe usijiambie tayari unajua, jifunze, hata kama unarudia kujifunza kitu, utaelewa zaidi kwa kurudia kujifunza.

NGUVU.
Mwanafalsafa Seneca amewahi kusema utawala ulio mkuu, ni kujitawala wewe mwenyewe.
Na hapo pia ndipo nguvu zetu zinaanzia, kwenye kujitawala na kujidhibiti mwenyewe.
Hata kama uko juu ya wengine wote, kama huwezi kujitawala na kujidhibiti mwenyewe, utaishia kuwa dhaifu tu.
Tamaa zako za mwili zitakudhalilisha na kukuzuia usipate kile unachotaka.
Jidhibiti na kujitawala wewe mwenyewe na utaweza kuotawala dunia nzima.

UTAJIRI.
Wengi hufikiri utajiri ni kupata zaidi na zaidi,
Lakini changamoto ni kwamba, tamaa ya kutaka zaidi haijawahi kushiba,
Ukiwa unatembea kwa miguu utatamani baiskeli, ukipata baiskeli utatamani pikipiki, ukishaipata utatamani gari, ukiipata utatamani kupata gari nyingine ya kifahari zaidi.
Hakuna ubaya kwenye kutaka zaidi, lakini kama utadharau kile ulichonacho kwa sababu unataka zaidi ya hicho, hapo umeyaharibu maisha yako.
Kama wakati una baiskeli unaidharau na kusema pikipiki ndiyo ya maana, hata utakapoipata utaidharau na kusema gari ndiyo ya maana.
Hivyo basi, kwa maisha yako yote, hakuna utakachofurahia, kwa sababu kuna cha juu zaidi ya kile ulichonacho.
Utajiri wa kweli ni kufurahia kile ambacho tayari unacho.
Na unapokitumia vizuri, kinakupa kilicho bora zaidi.
Chochote ulichonacho sasa kifurahie, maana kuna wengi wangetamani sana kukipata ila hawakipati.

Jifunze kila wakati, jitawale mwenyewe na furahia kile ulichonacho,
Kanuni rahisi ya kuwa na maisha bora kila siku.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania