Unapowauliza watu kuhusu maoni yao kwenye jambo lolote lile, watakujibu kwa namna ya kukufurahisha, yaani watakujibu kile unachotaka kusikia, kama hakuna gharama yoyote wanayoingia.

Hivyo kama wale unaotaka wakupe maoni au mrejesho hawaingii gharama yoyote, hawatakupa majibu sahihi.

Na hili lipo sana kwenye utafiti wa masoko. Ukiwauliza watu kama watanunua bidhaa au huduma fulani unayotaka kuanzisha, wengi watakujibu ndiyo. Wanakujibu ndiyo ili tu kukuridhisha au ili usiendelee kuwasumbua.

Lakini ukienda mbali zaidi, kwa kila aliyekujibu ndiyo, unamwambia una bidhaa hizo kumi kwenye gari yako na ukataka wanunue, hapo sasa ndiyo utapata majibu ya kweli. Wengi waliokujibu watanunua, watakuja na sababu kwa nini hawawezi kununua kwa wakati huo. Haijalishi sababu ni nzuri kiasi gani, kama hawapo tayari kuinunua kwa wakati huo, hawapo tayari kuinunua kwa wakati wowote.

Hivyo kama unataka kupata majibu sahihi, kama unataka kujua watu wanaamini nini, kama unataka kujua msimamo halisi wa watu, basi weka gharama kwenye kile unachowapima nacho. Pale mtu anapokuwa kwenye nafasi ya kutengana na fedha zake, ndiyo anaonesha rangi yake halisi ni ipi.

Kama unapima chochote na huhusishi gharama, jua unapata majibu ya kukufurahisha wewe, na siyo majibu halisi ambayo watu wanayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha