Njia rahisi na ya uhakika ya kushindwa ni kujipima kwa matokeo unayopata.

Kwa njia hii utashindwa kwa sababu ni mara chache sana utapata matokeo ambayo unategemea kupata. Mara nyingi utapata matokeo ambayo hukutegemea kupata. Na kwa kuwa kipimo chako ni matokeo, basi utajiona umeshindwa na hutaendelea tena kufanya.

Njia sahihi kwako kujipima ni juhudi unazoweka, hatua unazochukua na viwango ulivyojiwekea. Kwa njia hii, kila wakati utaendelea kuchukua hatua na kujisukuma kuwa bora zaidi kwa sababu unajipima kwa viwango ulivyojiwekea. Iwe matokeo yatakuja unavyotaka au la, hutaacha kufanya, maana unajipima kwa ufanyaji na siyo matokeo.

Kwenye uandishi, kujipima kwa matokeo ni kuangalia wangapi wamependa kazi yako ya uandishi, kitu ambacho kinaweza kukukatisha tamaa mapema. Kujipima kwa juhudi unazoweka ni kupima maneno mangapi umeandika kwa siku au vitabu vingapi umeandika kwa muda uliojiwekea.

Kwenye michezo, kujipima kwa matokeo ni kuangalia ushindi ambao umepata, kitu ambacho kinaweza kukukatisha tamaa kwa sababu siyo mara zote utapata ushindi. Kujipima kwa juhudi ni kuangalia kiwango cha mazoezi na maandalizi ambayo unafanya kila wakati, ambapo utaendelea kuwa bora zaidi.

Hata kwenye kazi na biashara, kuangalia matokeo ya mwisho pekee itakukatisha tamaa sana, lakini kuangalia juhudi ambazo unaweka, itakupa moyo wa kuendelea kuweka juhudi.

Uzuri ni kwamba, ukikazana na juhudi, matokeo yanakuja yenyewe. Na hilo halitakukatisha tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha