“The initial joy on becoming free is better than being a king; it is more beautiful than going to heaven; it is more important than commanding whole worlds.” —BUDDHIST WISDOM

Furaha ya kuwa huru, ni zaidi ya kuwa mfalme,
Uhuru wako ni kitu muhimu kuliko vingine vyote kwenye maisha yako.
Ukishakuwa huru, unaweza kuyaishi maisha unayotaka wewe.

Kwa bahati mbaya sana, dhana ya uhuru ni moja ya vitu viwili ambavyo binadamu hatujawahi kuvielewa (kingine ni furaha).
Huwa tunafikiri uhuru ni kutokuwepo kwa utumwa au ukandamizwaji,
Tunaona uhuru ni pale tunapoweza kufanya kila tunachotaka.
Lakini hayo yote siyo sahihi.

Uhuru kamili ni pale unapojua nini unataka kwenye maisha yako, na kuwa tayari kuchukua hatua kupata hicho unachotaka, bila ya kujali wengine wanafanya nini au kusema nini.
Uhuru kamili ni kujua kusudi na maana ya maisha yako, kisha kuviishi hivyo kila siku, bila ya kuyumbishwa na yeyote.
Uhuru kamili ni pale unapojua mipaka na ukomo wako na kuzingatia.

Jamii haitaki wewe uwe huru,
Kwa sababu ukiwa huru utafanikiwa na kufanya makubwa,
Hivyo jamii inahakikisha inazuia uhuru wako, ili uwe kama wengine.
Ndiyo maana jamii inakupa hofu mbalimbali zinazokuzuia usifanye kile unachotaka au kujua ni sahihi kwako,
Jamii inahakikisha unafanana na wengine kwenye yale unayofanya.

Vita yako kuu ni kudai uhuru wako,
Kuusimamia kila siku na kuhakikisha hakuna anayeuingilia,
Kupuuza maoni ya wengi ambayo ndiyo sumu kwenye uhuru wako,
Kuzima matarajio ya wengine yanayokufanya uwe mtumwa kwao.
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kimeanzia ndani yako na kina maana kwako.

Maisha ni yako na uchaguzi ni wako,
Chagua kuwa huru na kuyaishi maisha yako,
Ndiyo njia pekee ya kuwa na maisha yenye furaha.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania