“If you see that an action is explained by a very sophisticated reasoning, then you can be sure that this action is bad. The decisions of the conscience are always strict and simple.” Leo Tolstoy

Ukiona mtu anaelezea kitu kwa maelezo mengi na mazuri kuliko inavyostahili, hapo jua kuna uovu unafichwa.
Ukiona mtu anatoa maelezo mengi kwenye swali linalohitaji jibu rahisi na la moja kwa moja kana ndiyo au hapana, basi jua ni uongo.
Matendo sahihi hayahitaji maelezo mengi ili kueleweka, yako wazi na kila mtu anajionea mwenyewe.
Ila matendo yasiyo sahihi lazima yaambatane na maelezo mengi, ili kumficha mtu uovu uliopo.
Kadhalika ukweli hauhitaji maelezo mengi ili kuonekana au kujulikana,
Ila uongo huwa unafichwa kwa maelezo mengi na mazuri.

Cha kusikitisha tumekuwa na jamii inayotufundisha kutumia muda mwingi kueleza tunachofanya, badala ya kuweka muda huo kwenye kufanya na matokeo yajioneshe yenyewe.
Tunatumia muda mwingi kuigiza kufanya, ili tuonekane ni wafanyaji, badala ya kupeleka nguvu na muda huo kwenye kufanya kweli ili matokeo yajioneshe yenyewe.

Kuwa mtu wakufanya na mara zote fanya kile kilicho sahihi.
Na hutakuwa na haja ya kutengeneza hadithi nyingi za kueleza nini umefanya,
Maana matokeo yatakuwa yanajionesha yenyewe.
Kumbuka ukiamua kudanganya, unakuwa umejidanganya mwenyewe.
Hivyo mara zote simama upande wa ukweli na fanya kilicho sahihi.
Na unapoulizwa, jibu kile ulichoulizwa na siyo kutoa maelezo mengi kwa lengo la kuficha uovu au uongo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania