Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Dune kilichoandikwa na Frank Herbet. Hii ni riwaya ya kisayansi (science fiction novel) ambayo iliandikwa mwaka 1965 na baadaye kufuatiwa na mfululizo wa riwaya nyingine zilizoendeleza visa hivyo.

Riwaya ya Dune inaelezea jamii ya kufikirika ya miaka 10,000 mpaka 20,000 ijayo. Katika zama hizo binadamu wamefikia uwezo wa kutawala ulimwengu mzima na kukalia kila sayari ulimwenguni.

Riwaya hii inaonesha familia tatu za kiuongozi ambazo zinagombania kushikilia sayari ya Arrakis ambalo ni jangwa lakini ina upatikanaji mkubwa wa viungo (spices melange) ambavyo ni dawa inayorefusha maisha na kumpa mtu uwezo mkubwa wa kufikiri.

Riwaya hii inagusa maeneo mbalimbali ya maisha ya wanadamu, kuanzia sayansi, anga, mazingira, ikolojia, dini, falsafa na siasa.

Riwaya kwa ufupi.

Mwaka 10,191 familia ya House Atreides ambayo inaongozwa na Duke Leto inaondoka kwenye sayari ya Caladan ambayo ndiyo makazi yake rasmi na kwenda sayari ya Arrakis, ambapo kwa utaratibu wa familia tatu, ilikuwa zamu yao kushika udhibiti wa sayari hiyo ambayo ndiyo chanzo pekee cha viungo (melange) vinavyotumika kama dawa.

Leto na familia yake, ambayo ina hawara yake Lady Jessica, mtoto wake wa kiume Paul na wasaidizi wake wengine wanaondoka Caladan kwenda Arrakis. Lakini Leto anagundua kwamba familia iliyokuwa inaishikilia Arrakis kabla ya zamu yao, ambayo ni House Harkonnen, ilikuwa imemuwekea mtego, ili imuue na kutokomeza kabisa familia yake.

Licha ya hatari hiyo, Leto anaenda Arrakis huku akiambatana na wasaidizi waaminifu kwake Thufir Hawat ambaye alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri (mentant) na Gurney Halleck aliyekuwa mbobezi wa silaha na muuaji mkuu. Wengine kwenye familia hiyo ni Wellington Yueh ambaye ni daktari na Duncan Idaho ambaye ni mpelelezi mkuu.

Arrakis ni jangwa ambalo wakazi wake wa asili wanaitwa Fremen, hawa ni watu ambao wamejifunza kuishi kwenye jangwa vizazi vyao vyote, hivyo wana mbinu mbalimbali za kuwawezesha kuendesha maisha jangwani, sehemu ambayo maji ni uhaba sana. Maji kwao ndiyo kitu chenye thamani kubwa na wana usemi kwamba nyama ni za mtu, ila maji ni ya jamii, hivyo mtu akifa anakamuliwa maji yake yote na yanatumika na wengine. Licha ya kuwa wakazi wa jangwa hilo, huwa hawajisumbui na viungo vinavyopatikana kwenye hilo jangwa na hivyo familia tatu zinazoongoza hazisumbuki nao sana.

Hawara (hajamuoa rasmi kwa sababu za kuepuka machafuko) wa Leto ambaye ni Lady Jessica ni mwanachama wa shule ya Bene Gesserit ambaye ana mafunzo yote na anampatia mtoto wake mafunzo hayo. Kabla ya kumzaa mtoto huyo wa kiume, shule yake ilimpangia azae mtoto wa kike, ili akaozeshwe kwenye familia ya Harkonnen na kuepusha mapigano baadaye. Lakini Jessica anaenda kinyume na maagizo ya shule yake, kitu ambacho kinaweka ulimwengu kwenye hatari ya kutokea machafuko kati ya familia hizo mbili.

Familia ya House Harkonnen inaongozwa na Baron Vladimir Harkonnen ambaye ana wapwa wawili, Feyd-Rautha, ambaye anaandaliwa kushika uongozi na Glossu Rabban ambaye ni msimamizi wa biashara ya viungo. Pia Baron ana msaidizi wake mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri (mentant) ambaye ni Piter De Vries.

Familia ya Corrino ndiyo inayotawala ulimwengu wote (the Imperium) na kiongozi mkuu ni Shaddam IV Padishah ambaye ana mabinti wa tano, ambapo binti yake mkubwa Princess Irulan ndiye anayeandaliwa kushika uongozi. Lakini pia Shaddam ana rafiki yake wa karibu na anayemwamini sana anayeitwa Count Hasimir Fenring, huyu ndiye anayemtumia kwa shughuli mbalimbali za kiuongozi.

Shaddam anaona Leto akiwa na ushawishi mkubwa na kuona baadaye anaweza kuja kushika kiti cha uongozi mkuu. Hivyo anashirikiana na familia ya Harkonnen kwa siri kumuua Leto na kuangamiza kizazi chake chote. Baron anaweka pandikizi kwenye familia ya Atreides ambaye ni Dr Yueh. Huyu ni daktari anayeaminika sana kutokana na shule aliyosomea na hivyo hakuna anayemhisi kama anaweza kuwa msaliti.

Dr Yueh anatengeneza mazingira ya Harkonnens kuvamia familia ya Atreides wakiwa Arrakis kwa kutumia msaada wa jeshi la siri la Shaddam linalojulikana kama Sardaukar. Leto anakamatwa na kuchukuliwa mateka, huku Yueh akiwasaidia Jessica na Paul kutoroka. Yueh anamwekea Leto jino la bandia ambalo ni sumu na kumwambia atakapokuwa na Baron alitafune ili wafe wote. Hilo linashindikana na Leto anakufa huku Baron akipona.

Jessica na Paul wanapotelea jangwani ambapo wanakutana na watu wa jamii ya Fremen ambao wanawapokea na kuishi nao. Jessica na Paul walikuwa na uwezo wa ajabu waliojifunza kupitia mafunzo ya shule ya Bene Gesserit ambayo wanawashirikisha Fremen huku wakijifunza jinsi ya kuishi kwenye mazingira ya jangwa kwa maji kidogo. Paul anatambua kwamba ana nguvu za tofauti na watu wa jamii ya Fremen wanamkubali sana na kumpokea kama masia, akitumia jina la Muad’Dib, anapata hawara aitwaye Chani na kuzaa naye  mtoto anayeitwa Leto II. Nguvu za tofauti alizo nazo Paul ni za juu kabisa kwenye shule ya Bene Gesserit ambapo anajulikana kama Kwisatz Haderach, mtu mwenye uwezo wa kuwa sehemu mbili kwa wakati mmoja na mwenye uwezo wa kuona mambo yajayo. Jessica naye anapewa nafasi ya heshima kwenye jamii hiyo kama mama kiongozi (Reverend Mother) kutokana na nguvu zake za ajabu za kuweza kusoma mawazo ya watu na kuwatawala watu kutumia sauti yake.

Baron kwa kuamini kwamba ameshaitokomeza familia ya Atreides, anajiona ndiye mmiliki mkuu wa Arrakis. Taarifa anazopata ni kwamba Jessica na Paul wamekufa wakati wanatorokea jangwani. Anamchukua aliyekuwa msaidizi wa Leto ambaye ni Thurit Hawat kuwa msaidizi wake. Kwa kutumia msaafa wa Hawat, Baron anapanga kumpindua Mtawala mkuu (Emperor) Shaddam na kumweka madarakani mpwa wake Feyd-Rautha.

Paul kwa sasa akiwa kiongozi mkubwa na mwenye ushawishi kwenye jamii ya Fremen, ambao wanamtukuza kama masia kwa, anaona fursa ya kutumia uwezo mkubwa wa jamii hiyo kuangusha utawala wa familia ya Harkonnen. Wanapanga kuvamia makao makuu ya Arrakis ambapo kwa wakati huo yanakaliwa na mpwa wa Baron ambaye ni Rabban.

Wakati huo huo kiongozi mkuu Shaddan anajua njama za Baron za kutaka kumpindua, hivyo yeye pamoja na jeshi lake la siri wanaenda Arrakis.

Paul kwa kushirikiana na wapiganaji wa Fremen, anafanikiwa kuwaua wanajeshi wengi wa kiongozi mkuu, huku mdogo wake Paul aitwaye Alia akimuua Baron mwenyewe.

Paul anakutana uso kwa uso na mtawala mkuu na kumtaka aachie madaraka la sivyo ataharibu mfumo mzima wa upatikanaji wa viungo dawa. Feyd-Rautha anajaribu kupambana na Paul lakini Paul anamshinda na kumuua.

Shaddan anakuwa hana namna bali kuachia ngazi yake na kumkabidhi Paul utawala wa ulimwengu (Emperor). Paul anachagua kumuoa binti wa Shaddan ambaye ni Princess Irulan, lakini ndoa hii ni ya kisiasa tu kuzuia machafuko, lakini mapenzi yake halisi ni kwa hawara yake aliyempata kutoka jamii ya Fremen.

Hivyo Paul anafikia lengo la kushika utawala wa ulimwengu, kwa nia ya kuzuia machafuko makubwa yasitokee. Lakini anakuwa ameshachelewa, kwa sababu nguvu yake kubwa imetengeneza wafuasi na hivyo kuwa kama dini. Hapo ndipo ulipo mwendelezo wa riwaya nyingine za Dune. Lakini kwa riwaya hii, inaishia pale Paul anapopata uongozi mkuu wa ulimwengu (Emperor of the Known Universe)

Karibu kwenye uchambuzi.

Karibu sana kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha Dune ambapo tunajifunza mengi sana kupitia visa vilivyopo kwenye riwaya hii. Riwaya hii unaweza kuisoma kwa mitazamo tofauti na kwa kila mtazamo ukajifunza vitu vipya.

Unaweza kuisoma kwa mtazamo wa kisayansi na hapa ukajifunza kuhusu mabara mbalimbali ya ulimwengu.

Unaweza kuisoma kwa mtazamo wa kisiasa na hapa ukajifunza mbinu mbalimbali za kiutawala na mapinduzi.

Unaweza kuisoma kwa mtazamo wa kidini na hapa ukajifunza jinsi mtu anavyoweza kuanzia chini mpaka kufikia kutukuzwa kama masia na watu kumwamini sana.

Unaweza kuisoma kwa mtazamo wa mazingira na ikolojia na ukajifunza jinsi jangwa linavyoweza kubadilishwa na kuwa sehemu rafiki kwa maisha.

Unaweza kuisoma kwa mtazamo wa ugumu na ubunifu wa binadamu na ukajifunza jinsi watu wanavyoweza kuishi kwenye mazingira magumu.

Unaweza kuisoma kwa mtazamo wa upangaji wa uzazi na kujifunza jinsi mpango unavyoweza kushindwa na kuleta madhara makubwa.

Hii ni riwaya ambayo unajifunza kila kitu kuhusu maisha, na hivyo itatusaidia sana kwenye safari yetu ya maisha ya mafanikio.

Tutakuwa na chambuzi tatu za vitabu vitatu vilivyopo kwenye riwaya hii ambavyo ni DUNE, MUAD’DIB na THE PROPHET. Karibu tujifunze na kutumia yale tunayojifunza kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

Kupata uchambuzi za kina wa kitabu hiki na vitabu vingine vingi, jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail  

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania