Kwenye biashara, ni rahisi kila mtu kupunguza bei ya kile anachouza ili kuvutia wateja zaidi. Lakini mmoja akishapunguza, mwingine naye anapunguza. Hivyo mashindano yanakuwa ni nani anayeweza kuuza kwa bei rahisi zaidi. Wote mnaoshindana mnaishia kuumia, huku mteja akipata manufaa yote.
Kama umeingia kwenye biashara kwa malengo ya muda mrefu, kama ndiyo kitu ambacho umechagua kweli kufanya, basi epuka sana njia hiyo ya urahisi.
Badala yake tumia njia ya ubunifu. Tafuta kitu cha tofauti unachoweza kufanya kwenye biashara yako, ambacho wengine hawawezi kufanya kisha fanya hicho.
Hatua ya kwanza kabisa kwenye ubunifu ni kuchagua wateja wachache ambao biashara yako inawalenga. Huwezi kuwa mbunifu kama unamlenga kila mtu, bali unaweza kuwa mbunifu kama utawalenga wachache wenye sifa fulani ambayo unaweza kuwapatia.
Hivyo andaa bidhaa au huduma ambayo inawalenga wachache, kisha weka bei ambayo wataweza kuimudu na pia itakupa wewe faida ya kukuwezesha kuendelea na biashara hiyo bila ya kuhangaika na vitu vingine.
Baada ya hapo kuwa na njia ya masoko ambayo itawafikia wateja unaowalenga na kuweza kuwashawishi kununua kile unachouza. Hutawashawishi kwa urahisi, bali kwa kile wanachoweza kupata kwako, ambacho hawawezi kupata kwa wengine.
Usikazane kuwa rahisi, badala yake kazana kuwa mbunifu. Urahisi utakuumiza kwa sababu hata ukishinda, kuna mwingine anaweza kuwa rahisi zaidi yako. Lakini kwenye ubunifu, kadiri unavyokuwa mbunifu, ndivyo unavyonufaika zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kabisa Kocha,kwa mfano katika biashara yetu ya bookkeeping na advisory unapochagua kuwahudumia wateja kwenye specific industry kwa mfano unafocus kuwahudumia service providers then unakwenda mbali zaidi labda kuwahudumia wateja katika sekta ya hospitality.Hii inakufanya upate nafasi ya kuijua industry kwa undani zaidi ,hivyo kuwapatia wateja wako huduma za kibunifu na bora zaidi.
LikeLike
Kabisa Hafidhi,
Wengi hufikiri ukishakuwa na taaluma basi unaweza kumhudumia kila mtu, ni kweli lakini utakosa ubora.
Ukichagua aina fulani ya wateja na ukawahudumia vizuri, unatoa kazi bora na hivyo kulipa vizuri pia.
LikeLike
Asante sana Kocha kwa hili somo. Ni kweli ninatakiwa kuwa mbunifu kwenye kutoa huduma na sio kulenga tu kuwa rahisi.
LikeLike
Vizuri.
LikeLike