Kama umwahi kujikuta njia panda, ukijiuliza ni nini unapaswa kufanya, jua kwamba kinachokukwamisha siyo kutokujua cha kufanya, bali utayari wako kwenye kukifanya.

Katika kila hali unayopitia, unachopaswa kufanya ni kile sahihi kufanya. Na kwa kila hali, kuna vitu ambavyo ukifanya, haviwezi kuharibu chochote bali vitafanya hali yako iwe nzuri.

Kwanza kabisa ifanye kazi yako kwa juhudi. Hivyo unapojikuta njia panda, jiulize kazi yako ni nini, kisha fanya hiyo. Kama upo kwenye biashara kazi yako ni kuwahudumia wateja wako vizuri, fanya hivyo kwa juhudi kubwa. Kama ni mwalimu kazi yako ni kufundisha, fanya hivyo. Kadhalika kwa kazi na biashara nyingine.

Pili kuwa mwaminifu, hata kama mambo ni mabaya kiasi gani, uaminifu hauwezi kuyafanya mambo kuwa mabaya zaidi, badala yake utarahisisha mengi. Mara zote kaa upande wa ukweli, usijaribu kuficha chochote, unapokuwa njia panda ni rahisi kuamini kuficha vitu kutasaidia, lakini hilo hupelekea mambo kuwa mabaya zaidi baadaye. Kuwa mwaminifu, kuwa upande wa ukweli, tekeleza ulichoahidi na usifanye chochote kisicho sahihi.

Tatu wasaidie wengine. Pale unapojikuta njia panda ambapo umekwama kabisa na unaona huna unachoweza kufanya, acha kujiangalia wewe na angalia wengine. Jiulize ni mtu gani unayeweza kumsaidia, kisha fanya hivyo. Kwa kusaidia watu wengine, kwanza utasahau ulipokwama wewe kwa muda, pili utagundua wengine nao wamekwama kama wewe na tatu utapata njia ya kutoka pale ulipokwama. Unaweza kuanza biashara kwa njia hiyo, kadhalika unaweza kupata kazi kupitia kuwasaidia wengine.

Kamwe usikae ukiwa huna unachofanya kwa sababu umejikuta njia panda na hujui nini ufanye. Badala yake fanya kazi yako kwa juhudi, kuwa mwaminifu na wasaidie wengine kuondoka pale walipokwama. Fanya mambo hayo matatu na maisha yako yatakuwa bora kila wakati, hata kama unapotia magumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha