Mkulima anapaswa kulima shamba, kupanda mazao, kuyapalilia, kuweka mbolea, kupalilia tena na kisha kusubiri yakomae ndiyo ayavune. Kwa njia hii anahitaji kujenga mahusiano ya karibu na kile anachofanya, anapokwenda kulala anafikiria mazao yake, mvua ikiwa nyingi au kidogo anafikiria mazao yake na hili linamfanya ajitoe zaidi na katika kujitoa huko anafanikiwa kwa kupata mazao mengi.

Mwindaji kwa upande mwingine anaangalia mnyama anayepita mbele yake na kumwinda, atakimbizana na mnyama huyo mpaka amkamate au kumuua na hapo kazi imeisha. Kesho atatafuta tena mnyama mwingine. Mwindaji hajengi mahusiano yoyote na kazi yake, halei mnyama mdogo mpaka akue ili aje kumwinda baadaye, yeye anaangalia yule ambaye yuko tayari. Wakati mwingine mwindaji anaweza kuachana na mnyama aliyekuwa anamlenga kama ameona mnyama mwingine ambaye atakuwa na manufaa kwake kuliko aliyekuwa anamlenga awali.

Hizo ndiyo njia mbili za kuchagua jinsi ya kufanya kazi au biashara yako.

Unaweza kuchagua kufanya kama mkulima, kwa kutengeneza mahusiano mazuri na wateja wako na kwenda nao kwa muda mrefu. Njia hii inahitaji kazi kama ilivyo kwa mkulima, lakini ina manufaa makubwa ukishatengeneza watu sahihi wa kwenda nao.

Au unaweza kuchagua kufanya kama mwindaji, kwa kuchagua kumhudumia mteja mara moja na kuachana naye, kisha kutafuta mwingine mpya. Kila mara unakimbizana na vitu vipya na huna muda wa kwenda na kitu kimoja kwa muda mrefu. Njia hii haihitaji kazi sana, lakini inakuchosha, kwani muda unavyozidi kwenda unajikuta huna ulichotengeneza ambacho unaweza kukitegemea.

Kwa dunia tunayoishi na kwa namna maisha yetu yanavyokwenda, ni vyema kuweka nguvu mwanzoni katika kujenga mahusiano mazuri na wale wanaotegemea kazi zako, na baadaye inakuwa rahisi kukuza watu hao na kufikia wengi zaidi huku ukiwa huna wasiwasi wa kutakiwa kuanza upya kila wakati.

Kwa chochote unachofanya, chagua kuwa mkulima, chagua kuweka kazi, chagua kuwa na subira na mambo yatakuwa mazuri kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha