“Be strict in judging yourself and gentle in judging others, and you will have no enemies.” — CHINESE WISDOM
Kama hutaki maadui kwenye maisha yako,
Kuwa mkali kwenye kujihukumu mwenyewe na mpole kwenye kuhukumu wengine.
Sisi binadamu huwa hatuoni kitu kama kilivyo, bali huwa tunakiona kama tunavyokihukumu.
Yaani tunaanza kwa kuhukumu kwanza kabla ya kufanya maamuzi mengine.
Na hukumu nyingi tunazowapa watu zinakuwa siyo sahihi,
Kwa sababu kuna mengi hatujui kuhusu watu hao.
Chukua mfano umemsalimia mtu na hakuitika,
Moja kwa moja unakwenda kwenye hukumu,
Utajiambia ana dharau, au amekununia, utakumbuka mpaka mambo ambayo mlipishana siku za nyuma na kuamini ndiyo yamefanya asiitikie salamu yako.
Utahukumu hivyo na kisha utafikia maamuzu, sitomsalimia tena mtu huyu maana ananidharau au ameninunia.
Lakini kumbe wakati unamsalimia hakusikia, alikuwa na mawazo makali kutokana na mambo fulani ambayo hayaendi vizuri kwenye maisha yake, hivyo licha ya kuwa karibu kabisa, lakini akili yake ilikuwa mbali mno.
Hukumu uliyopitisha itajenga uadui kwa jambo ambalo halikuhitaji uadui.
Haijalishi mtu amefanya nini au kusema nini, jizuie kuhukumu kabla hujajua kwa undani nini kimempelekea yeye kufanya kitu hicho.
Watu wawili wanapokosana, tunaposikia hadithi ya upande mmoja tunaona wazi kwamba upande wa pili ulikosea sana.
Lakini ukija kusikia hadithi ya upande wa pili, unagundua upande wa kwanza nao ulikuwa na makosa pia.
Unaweza kujihukumu wewe mwenyewe kwa ukali kabisa,
Kwa kuwa unajijua vizuri, unajua nini ulipanga na hujafanya, unajua pale unapokuwa na hisia za wivu au chuki au kinyongo.
Unajijua, hivyo kujihukumu utakuwa sawa, na itakuwa njia ya wewe kubadilika.
Lakini kuhukumu wengine, mara zote unaishia kufanya makosa, maana huwajui watu hao kwa undani, hujui nini wanapitia na huwezi kujua msukumo hasa wa wao kufanya walichofanya.
Epuka kuhukumu wengine na utakuwa na utulivu na kupunguza uadui na watu.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania