Utangulizi.
A Journal of the Plague Year ni kitabu kilichoandikwa na Daniel Defoe mwaka 1712 kikieleza matukio ya pigo la ugonjwa wa tauni ambalo liliukumba mji wa London kati ya mwaka 1665 mpaka 1666. Pigo hili lilipelekea vifo vya watu zaidi ya laki moja na kuleta madhara makubwa kwenye mji wa London.

Daniel Defoe ameandika kitabu hiki kama mtu anayesimulia yale aliyoyashuhudia wakati wa mlipuko huo wa tauni. Lakini wakati mlipuko unatokea, Defoe alikuwa na umri wa miaka 5 hivyo asingeweza kuwa na kumbukumbu sahihi.
Hivyo inaonekana Defoe alifanya utafiti na kujua yale yaliyoendelea wakati huo wa mlipuko, kisha akaandika kama mtu anayesimulia. Lakini pia inawezekana Defoe aliandika kitabu hiki kupitia jarida la mtu aliyeishi kipindi cha mlipuko. Hakuna mwenye uhakika wa chanzo cha hadithi hii, lakini wanahistoria wanakubali kwamba hii ni hadithi inayoeleza kwa ukweli sana matukio ya mlipuko huo wa tauni mjini London.
Mwanzo wa kitabu Defoe ameandika; kumbukumbu ya matukio yaliyotokea wakati wa mlipuko wa tauni 1665 ambayo imeandikwa na mwananchi ambaye alikuwepo London kipindi chote cha mlipuko. Mwisho wa kitabu ameweka sahihi H.F kama mwandishi wa jarida hilo.
Pamoja na ukweli wa chanzo cha hadithi kutokujulikana, imebeba uhalisia wa matukio hayo. Kwa sababu Defoe amejumuisha taarifa na takwimu mbalimbali ambazo zilikuwa zinatolewa na sharika pamoja na ofisi za serikali wakati wa mlipuko huo.
A Journal of the Plague Year ni moja ya vitabu ambavyo tunaweza kujifunza mengi kuhusu milipuko ya magonjwa na hata majanga mengine ambayo yanaleta madhara kwa watu wengi. Kitabu hiki kinatufundisha jinsi baadhi ya hatua ambazo zinachukuliwa na umma, pamoja na mtu binafsi zinavyoweza kuwa na madhara wakati wa mlipuko.
Na kikubwa zaidi, kitabu kinatufundisha kwamba wakati wa mlipuko au majanga yoyote, njia bora ya kusalimika ni kutokutaharuki, kuchukua tahadhari ambazo zinatolewa na wataalamu na kuomba kulingana na imani yako. Kupitia msimuliaji, tunajifunza mengi ambayo tukiyajua na kuyafanyia kazi yatatusaidia sana kwenye maisha.
Kuanza kwa mlipuko.
Mwanzoni mwa mwezi Septemba 1664 taarifa zilianza kusambaa London kwamba kuna mlipuko wa tauni nchini Holland. Taarifa zilisema mlipuko huo ulikuwa umeanzia Italy, nyingine nikisema Uturuki na kadhalika na mlipuko huo ulisambaa kwa njia ya safari za meli.
Kwa kuwa hakukuwa na magazeti kipindi hicho, njia pekee ya kupata habari ilikuwa kupitia barua ambazo wafanyabiashara wa nchi mbalimbali walikuwa wakiandikiana.
Baada ya tetesi za mlipuko huo wa tauni kuanza kusambaa, ilionekana kama serikali imejipanga kukabiliana nao, kwani vikao mbalimbali vilifanyika kwa siri. Tetesi hizo zilipotea na watu kuendelea na maisha kama kawaida.
Mwishoni mwa mwezi Novemba na mwanzoni mwa mwezi Disemba 1664 watu wawili wa familia moja walifariki kwa ugonjwa wa tauni. Familia ya watu hao ilificha taarifa za vifo vyao na kufanya siri. Lakini serikali ilipata taarifa na kuunda kamati ya madaktari ambao walifanya uchunguzi kwa miili ya waliokufa. Katika uchunguzi wao, waligundua marehemu walikuwa na uvimbe kwenye ngozi, ambayo ni dalili kuu ya tauni, na hivyo kuthibitisha kwamba watu hao walikufa kwa tauni.
Baada ya taarifa hizi kutoka kwamba London kuna watu wamekufa kwa tauni, watu walianza kuchukua tahadhari kubwa. Wiki ya mwisho ya mwezi Disemba 1664 mtu mwingine alikufa kwenye familia ile ile ambayo watu wawili walikufa kwa tauni.
Baada ya hapo, kwa wiki sita hakukuwa na kifo kingine, na hapo watu wakaanza kurudi kwenye maisha ya kawaida na kuamini hakuna tauni, kama ilikuwepo basi ilipita tu. Mwezi Februari 1665, mtu mwingine alikufa kwenye nyumba nyingine, lakini eneo lile lile ambalo watu wa mwanzo walikufa, na dalili zilikuwa zinafanana.
Taarifa za vifo kwenye maeneo mengine zilianza kuongezeka, idadi ya vifo kwa wiki ilianza kuwa kubwa kuliko kawaida na vifo vipya vilikuwa vya dalili za tauni.
Mlipuko huo uliendelea kukua na kupungua kwa kipindi cha miezi ya mwanzo ya mwaka 1665 na hii iliwafanya watu kutokuwa na uhakika kama ni mlipuko kamili wa tauni au la.
Mambo ya kujifunza na kufanyia kazi.
Licha ya kwamba mwandishi au usahihi wa simulizi hii ya mwaka wa tauni haujulikani, lakini matukio yaliyoelezwa, wanahistoria wanakubali kwamba yanaendana sana na kile kilichotokea.
Kwa kuwa tunaishi kwenye dunia yenye milipuko ya magonjwa mbalimbali, kuna mengi ya kujifunza na kuyafanyia kazi pale tunapokuwa kwenye mlipuko wa aina hii. Kwa kujumuisha, haya ni ya msingi kabisa kufanya.
1. Kujua chanzo na kusambaa kwa mlipuko, hii itasaidia kujikinga.
2. Kuepuka kukutana na watu au vitu vyenye mlipuko. Kama unaweza ondoka eneo lenye mlipuko, kama huwezi jifungie ndani na yeyote asiingie wala kutoka.
3. Epuka kusikiliza watabiri na wengine wanaojitangaza wana dawa za mlipuko uliotokea. Dawa huwa zinachukua muda mpaka kupatikana, njia sahihi wakati wa mlipuko ni kujikinga.
4. Kuhakikisha kila wakati una maandalizi ya kutosha, hata kabla ya mlipuko kutokea. Mfano kuwa na akiba ya kutosha ili mlipuko unapotokea usiwe na ulazima wa kuendelea na shughuli zako kuingiza kipato.
5. Kuepuka kusambaza ugonjwa kwa wengine pale unapoupata au ukigundua umekutana na mwenye nao basi kujitenga na kuangalia kwanza hali yako inaendaje.
6. Kutoa msaada kwa wale wasiokuwa na uwezo ili waweze kupata mahitaji yao na kutolazimika kuendelea na shughuli zao.
7. Kufuata ushauri wa kitaalamu unaotolewa kulingana na mlipuko husika na kisha kutekeleza ushauri huo ili kuzuia kupata na hata unapoupata kuchukua hatua sahihi.
8. Amini lakini chukua tahadhari, usijiambie Mungu atakulinda huku unaendelea kuchukua hatua za hatari zinazokuweka kwenye hali ya kupata ugonjwa wa mlipuko.
9. Kutokushangilia mapema kwamba mlipuko umeisha kwa sababu vifo au wagonjwa wamepungua, badala yake kuendelea na tahadhari hata baada ya mlipuko kuonekana umeisha. Maana milipuko ina tabia ya kuwa na awamu ya pili ya maambukizi.
10. Kumbuka kwamba milipuko ipo na itaendelea kuwepo, kwa historia dunia imepitia milipuko mingi, huwa inaisha na baadaye kuja kuibuka tena, hivyo tusijisahau, badala yake tuwe na maandalizi wakati wote.
Karibu usome uchambuzi kamili.
Karibu usome uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha A Journal of the Plague Year ambapo mtindo tutakaotumia ni kuenda na simulizi kama mwandishi anavyosimulia kwa kuchagua yale muhimu ambayo kuna vitu vya kujifunza na hatua tunazoweza kuchukua ili kufanya maamuzi bora kwenye maisha yetu, hasa nyakati za majanga.
Kuupata uchambuzi wa kina wa kitabu hicho na vingine vingi, jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania