Dalali akitaka ununue au kulipia kitu, huwa anakutengenezea njia ya kufanya ulinganisho, ambao utakupelekea kufanya maamuzi anayotaka yeye.

Chukua mfano unataka kupanga nyumba na unaenda kwa dalali, ambaye unamweleza mahitaji yako kwenye nyumba unayotaka kupanga. Moja kwa moja atajua katika nyumba alizonazo ipi itakufaa.

Lakini hatakupeleka kwenye nyumba ile moja kwa moja. Bali atakachofanya ataanza kukuzungusha kwenye nyumba nyingine ambazo ni mbovu halafu hatakutajia bei ya ukweli, atataja bei za juu sana. Hilo litakukatisha tamaa, kuona nyumba za hovyo hivyo ni ghali.

Akishakupitisha kwenye nyumba tatu za aina hiyo, anakupeleka kwenye ile nyumba ambayo ndiyo anataka uichukue, na hapo utaona vitu viwili, cha kwanza ni nzuri ukilinganisha na zile tatu ulizoona awali na kitu cha pili bei yake itakuwa chini kuliko zile tatu za awali.

Hapo utaona umepata dili nzuri na hivyo kujiambia uchukue hatua haraka kabla hujakosa dili hiyo. Unalipia nyumba hiyo, kwa vigezo ambavyo siyo sahihi. Baadaye unapokuja kutulia, unagundua kuna nyumba nyingine nzuri kuliko hiyo, tena kwa bei ambayo ni nafuu zaidi.

Kilichotokea hapo ni udhaifu ambao upo kwenye saikolojia yetu binadamu, huwa hatuoni kitu kama kilivyo, bali huwa tunaona kitu kwa kuhukumu, na hukumu hiyo ni kwa kulinganisha na vitu vingine.

Hata kwenye mahusiano, unaweza kushindwana na mtu mmoja na kuanzisha mahusiano na mwingine, kwa sababu tu ukimlinganisha huyo mpya na wa zamani, mpya ana afadhali kidogo. Lakini baadaye mnakuja kushindwana tena.

Unapaswa kuvuka udhaifu huu wa kufanya maamuzi kwa kulinganisha vitu, badala yake fanya maamuzi kwa kukiangalia kitu chenyewe. Kwanza anza na sifa unazotaka, kisha angalia kitu chenyewe kama kina sifa hizo. Unapokuwa unaangalia kitu, sahau kabisa kuhusu vitu vingine. Kiangalie chenyewe kwa sifa zake na siyo kukilinganisha na vitu vingine.

Watu wengi wamekuwa wananufaika na wewe kwa tabia yako ya kulinganisha vitu, achana na tabia hiyo sasa ili uepuke kutumiwa na wengine kwa manufaa yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha