Kwenye ukurasa wa 1991 nimekuambia uko tayari kuanza, huhitaji kusubiri mpaka uwe mkamilifu, anzia hapo ulipo sasa na endelea kujifunza kadiri unavyokwenda.
Lakini najua unaweza kuacha kuanza kwa kisingizio kwamba huna zana za kuanza kufanya, kwamba inahitaji gharama kupata zana hizo na huwezi kumudu gharama hizo kwa sasa.
Niendelee kukuambia kwamba huko ni kujidanganya na kujifariji, kukimbia kuweka kazi ambayo unapaswa kuweka ili ufanikiwe.
Hapo ulipo, tayari una zana za kukutosha kuanza chochote unachotaka kuanza, bila ya kuhitaji kuingia gharama yoyote ile.
Unajiambia utaanza kuandika pale utakapoweza kununua kompyuta, unajidanganya tu rafiki. Watu wamekuwa wanaandika vitabu kwa zaidi ya miaka elfu 2 sasa, kompyuta zimekuwepo siyo ya miaka 100. Vitabu bora kabisa tunavyotumia kujifunza leo, viliandikwa bila ya msaada wa kompyuta. Anza hata na Biblia na Koran, hivi ni vitabu vilivyodumu miaka na miaka, lakini havikuandikwa kwa kompyuta wala teknolojia yoyote ile, vilianza kwa kuandikwa kwa mkono, kwanza kwenye mawe na udongo na baadaye kwenye karatasi. Naamini hapo ulipo unaweza kupata kalamu na karatasi kwa gharama za chini au bure kabisa, hivyo tumia zana hizo kuanza kuandika. Usiache mpaka upate kompyuta, anza na ulichonacho.
Unajiambia hutaanza biashara mpaka uweze kukodi fremu, uweze kununua mali na kuziweka kwenye eneo lako la biashara. Hivyo unasubiri upate mtaji ndiyo uanze biashara, hapa pia utajisubirisha sana. Kwa nini usianze na zana ambazo tayari zinakuzunguka, una watu wa karibu ambao wana malalamiko fulani, na wewe unajua jinsi ya kuyatatua, kwa nini usiwatatulie na wakakulipa. Labda ni mavazi, wakikuona umevaa wanakuambia umependeza, lakini wao hawawezi kuchagua au kupata mavazi mazuri kama yako. Kwa nini usiwaambie wakupe wewe fedha uende kuwachagulia mavazi mazuri kama yako, anza na mmoja, endelea na wengine na baada ya muda unakuwa kwenye biashara.
Unataka kuanza mazoezi, lakini unajiambia mpaka ununue vifaa, ukajiandikishe eneo la kufanyia mazoezi, uwe na nguo na viatu sahihi na mengine mengi. Unasubiri mpaka upate yote hayo. Kwani hapo unapokaa hakuna njia unayoweza kuzunguka kila siku kwa kukimbia? Kwani huwezi kuchukua kamba yoyote na kuanza kuruka. Zana zimekuzunguka, ni wewe tu unataka kujizungusha ili usianze.
Rafiki yangu mpendwa, kama umekuwa unanielewa, unajua kabisa nisichotaka ni wewe uniambie sijaanza kwa sababu sina hiki au kile. Nitakuacha ukiniambia sijaanza kwa sababu sitaki kuanza, lakini ukinipa sababu nyingine yoyote ile, nitakuonesha wazi kwamba unajidanganya.
Anza sasa kile ambacho umekuwa unajizungusha kuanza, au jiambie wazi kwamba hutaki kuanza. Kujidanganya hakutakusaidia kwa namna yoyote ile.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,