“If someone succeeds in provoking you, realize that your mind is complicit in the provocation.” – Epictetus

Kama umekasirishwa kwa namna yoyote ile, jua kabisa aliyekukasirisha ni wewe mwenyewe.
Kama umedharauliwa na wengine, jua wa kwanza kukudharau ni wewe mwenyewe.
Hakuna mtu yeyote mwenye nguvu ya kufanya chochote kwenye maisha yako, kama wewe mwenyewe hutampa nafasi ya kufanya hivyo.
Unakasirishwa kwa sababu akili yako imepima vitu vilivyosemwa au kufanywa na wengine kwa namna fulani.
Unaona umedharauliwa kwa jinsi akili yako imetafsiri maneno na matendo ya wengine.

Ukibadili mtazamo ulionao na jinsi unavyoyachukulia maisha,
Ukishika hatamu ya maisha yako mwenyewe,
Unamnyima kila mtu nguvu ya kukukasirisha au kukudharau.

Zipo njia mbalimbali za kufanya hili,
👉🏼Moja ni kubadili mtazamo wako kuhusu maisha na watu wengine pia, usiwaone wapo kwa ajili ya kukushambulia wewe, bali waone wanahangaika na maisha yao.
👉🏼Mbili ni kupuuza yale usiyoyataka, kama mtu amefanya au kusema kitu ambacho hukubaliani nacho, kipuuze. Chukulia kama hujaona au hujasikia, chukulia kwamba amefanya bila kujua hata kama amekusudia. Kupuuza kuna nguvu ya kumfanya hata aliyekusudia kuumia zaidi mwenyewe kuliko wewe.
👉🏼Tatu ni huruma, kwa kuwaonea huruma wale wanaofanya mambo yanayokukwaza, hutaweza kukwazika. Ona ni watu wasiokuwa na uelewa, wachukulie kama watoto wadogo. Mtoto mdogo akikuambia kitu hakiwezi kukukasirisha wala kukuumiza, maana unajua ni mtoto tu huyo, hajui asemalo au afanyalo. Wachukulie na watu wazima hivyo pia, na hutakasirishwa au kuumizwa na chochote.

Kabla hujasema wengine wamekukasirisha, wamekukwaza au kukuumiza, jikumbushe kwamba wewe ndiye wa kwanza kujifanyia hivyo, wewe umewapa ushirikiano wa kutosha kukamilisha hilo.
Acha kuwapa ushirikiano na hutasumbuliwa na mambo hayo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania