Njia sahihi ya kufanikiwa huwa iko wazi na inaeleweka kirahisi na mtu yeyote yule.

Ukiona kuna njia ya mafanikio ambayo huielewi, ambayo una wasiwasi na usahihi wake, basi jua uko sahihi, kwamba njia hiyo siyo sahihi.

Hii ni kanuni fupi na rahisi sana itakayokuepusha na matatizo mengi kwenye maisha yako. Itakuzuia usiibiwe wala kutapeliwa, kwa sababu mipango yote ya kitapeli huwa inakuwa na walakini mwanzoni. Lakini tamaa huwa inakuzidi, unaingia na kuishia kupoteza.

Jiwekee leo msingi huu na uishi kila kitu, unapokuwa na wasiwasi au mashaka na kitu chochote kile, basi jiambie uko sahihi, mashaka hayo ni kweli na hivyo kiepuke.

Kwa msingi huu, kuna baadhi ya fursa utazikosa, lakini utanufaika kwa yale yasiyo sahihi utakayoyakwepa kuliko hasara unayopata kwa kukosa yaliyo sahihi.

Kwa zama tunazoishi sasa, zama za usumbufu mkubwa, zama za taarifa nyingi zinazochanganya na kukinzana, msingi huu ni muhimu na utakusaidia. Kama umeelezwa kuhusu fursa na hujaelewa kwa kina au una wasiwasi na fursa hiyo, basi achana nayo. Wala isikuume roho kwamba umepitwa na fursa nzuri au unakosa nafasi ya kunufaika, badala yake weka nguvu zako kwenye yale sahihi kwako kufanya.

Kwenye maisha ya mafanikio, chagua nini unataka na kisha peleka muda wako wote kwenye kuweka juhudi ili uweze kupata unachotaka. Unapokutana na fursa zinazoendana na kile unachofanyia kazi, jiulize kama umeelewa na kama huna wasiwasi wowote juu ya fursa hizo. Kwa kuwa utakuwa umewekeza muda mwingi kwenye eneo hilo, utakuwa na uelewa mpana. Hivyo kama kitu kinakupa wasiwasi, jua siyo sahihi na achana nacho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha