Ulipata kazi ya kwanza, ikawa hailipi vizuri, ukaicha. Ukapata nyingine, bosi akawa anakunyanyasa, ukaiacha pia. Ukapata nyingine, hiyo ukawa huelewi na wafanyakazi wengine, nayo ukaiacha pia. Na bado unalalamika kwamba hupati kazi nzuri. Hushtuki tu?

Umepata mwenza wa kwanza, tabia mkawa hamuendani, mkaachana, ukapata wa pili, tena mkashindwa kuelewana, ukapata wa tatu, mambo yakawa ni yale yale. Unalalamika kwamba hupati wenza sahihi. Hutaki kuuangalia ukweli?

Umeanza biashara ya kwanza, ikafa kwa sababu ya ushindani. Ukaanzisha nyingine nayo ikafa kwa sababu uchumi haukuwa mzuri. Ukaanzisha nyingine tena nayo ikafa. Unaujasiri kabisa wa kusema umejaribu kila biashara lakini hazifanikiwi.

Unaweza kuendelea kujipa mifano mingi ya vitu ambavyo umejaribu mara nyingi na vikashindikana, lakini ujumbe ninaotaka uupate ni huu. Kama umebadili vitu zaidi ya viwili na vikashindwa, tatizo siyo vitu hivyo, tatizo ni wewe.

Kama tatizo lingekuwa vitu hivyo, unapobadili basi tungetegemea upate matokeo mazuri. Lakini unabadili vitu hivyo, huku wewe ukiwa umebaki vile vile na ndiyo maana matokeo yanaendelea kubaki vile vile.

Unapaswa kuuangalia ukweli mchungu kama ulivyo, kwamba kitu pekee ambacho kipo kwenye kila jambo unaloshindwa ni wewe.

Kama hutakubali ukweli huo na kuchukua hatua sahihi, utaishia kurudia makosa yale yale na kupata matokeo yale yale.

Upo usemi kwamba mtu mmoja akikuambia wewe ni tatizo ana wivu na wewe, watu watatu wakikuambia wewe ni tatizo wanataka kukuhujumu, lakini watu kumi wakisema wewe ni tatizo, basi kweli wewe ni tatizo.

Kadhalika kwenye mambo unayokosea, unapokosea mara ya kwanza, kitu hicho kina tatizo, ukikosea mara mbili, hujakielewa vizuri, ukikosea mara tatu, una tatizo.

Ukabili ukweli ili uweze kuchukua hatua sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha